“Muende mkapate Upendo na Nguvu ya Roho Mtakatifu ili mkatumike kwa furaha na uaminifu” hayo aliyasema Askofu Dkt. Strohn Bedford Heinrich wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Bavaria nchini Ujerumani alipokuwa akihubiri kwenye mahafali ya 69 ya wanafunzi wa Chuo cha Biblia na Thelogia Mwika Oktoba 22, 2022.
Askofu Heinrich anasema ni siku muhimu kwa wahitimu hao na ni wakati sahihi kwao kwa kuwa wamekwishaandaliwa kuwaendea na kuwagusa watu wa Mungu kwa njia ya nyimbo na mahubiri wakiutangaza upendo wa Mungu kwa watu wote.
“Tuwe mabalozi wa uzima, tuonyeshe upendo penye chuki na mafarakano, penye huzuni, na machozi kwa ndugu zetu na kuwa faraja kwao”. Askofu Heinrich aliwaasa wahitimu hao.
Pia alisema tunapaswa kuwatetea wale wanoonewa na kunyanyaswa na vilevile kuwa chumvi ya ulimwengu.
Kawataka wakristo kuombeana na kusaidiana na kuishi maisha ya ushuhuda kuhusu Yesu na uzima.
“Tuendelee kuishi natumaini na imani kwamba Yesu yupo pamoja nasi siku zote na hakuna kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu, tuimbe tufurahi na tusisahau kamwe kuwa popote pale tulipo sisi ni kaka na dada ndani ya Kristo” Alihitimisha mahubiri yake Askofu Heinrich.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, akitoa salam zake, alimshukuru Mungu kwa mahafali ya 69 ya wahitimu hao na kuwapongeza wahitimu na waalimu kwa hatua waliyofikia.
Anasema Chuo cha Biblia na Theologia Mwika kimekuwa cha kihistoria katika kuwandaa watumishi wa Kanisa hapa nchini na nje ya nchi.
Ansema watumishi wanaohitimu katika chuo hicho wamekuwa wa mfano wa kuigwa katika mwenendo na tabia.
“Niwaombe wakufunzi na watumishi wote wa chuo hiki endeleeni kuwaanda watumishi ambao watakuwa mfano mzuri wanaolishika na kufundisha neno la Mungu na wenye kutunza urithi wa kilutheri”. Alisema Dkt. Shoo.
Aidha alitoa wito kwa wahitimu hao waende kwenye utumishi na huduma waliyoitiwa na Mungu na kutumika kwa uaminifu wakitambua nguvu yao itatoka kwa Yesu aliyekufa pale msalabni kwa ajili yetu.
“Muwapende wale mnaowahudumia na kuwahudumia kwa bidii kama wafuasi wa Yesu Kristo; Msiende kufanya mambo ya usanii kama wanaofanya baadhi ya watumishi. Msiende kuwa washerehekeshaji bali muende mkatumike ile huduma mliyoitiwa”. Alisema Dkt. Shoo.
Mkuu wa Chuo Mch. Obed Akyoo, akizungumza kuhusu chuo hicho kabla ya wahitimu kutunukiwa vyeti vyao, alisema chuo hicho kina kabiliwa na changamoto ya upungufu wa bweni la wanawake, chakula chakutosheleza kutokana na ukame, barabara ya kuingia chuoni na zile za ndani ya chuo, maktaba miundombinu ya uneme na maji.
Hata hivyo alisema mpango wa mbeleni ni kupanua bweni la wanawake, kuinarisha kitengo cha utafiti kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika kanisa kwa sasa na kuendeleza watumishi kitaaluma.
Julm ya wahitimu 86 wamehitimu katika kozi mbailimbali. Kati yao wanafunzi 40 wamehitimu kozi ya Elimu ya Kikristo na Uinjilist ngazi ya cheti, 17 kozi ya Wasaidizi wa Sharika huduma za jamii ngazi ya cheti, 6 Muziki Wa Kanisa ngazi ya cheti, 2 Stashahada ya muziki Kanisa na 21 theologia katika ngazi ya cheti.