BCC Kituo Kipya Moshi Mjini

Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi. Ni neno kutoka kitabu cha Injili ya Mathayo Mtakatifu sura ya 25 mstari wa 40 alilolisoma Mchungaji Mathayo Mtui katika ibada fupi ya kufungua kituo cha watoto wenye ulemavu wa akili usharika wa Moshi Mjini lilipokuwa Kanisa la zamani la Moshi Mjini

Mchungaji Mtui ambaye ni katibu wa idara  ya vijana Dayosisi ya Kaskazini aliyemwakilisha  Mhe. Msaidizi wa Askofu Mchungaji Deogratius Msanya katika mahubiri yake Septemba 6, 2022 alisema, Kanisa na jamii lina wajibu mkubwa wa kueneza nuru na upendo wa Mungu kwa kutenda matendo yaliyo mema kwa wahitaji na jamii.

Anasema Wakristo wanapaswa kuonyesha Ukristo wao kwa watu kwa matendo yao na si kwa kujitambulisha kwa maneno.

“Wakristo tunapaswa kufanya kwa vitendo na kupita katikati ya ulimwengu wenye giza na kuwa cheche na mwanga wenye kuleta nuru  kwa watu wenye shida na mahitaji” Alisema Mch. Mtui.

Aidha alipongeza kitengo cha Building a Caring Community (BCC) kwa jitihada wanazofanya za kuwahudumia watoto hao wenye ulemavu wa akili katika sharika za Manispaa ya Moshi.

Kabla ya ufunguzi rasmi Mhe. Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebadiah Moshi alipongeza usharika wa Moshi mjini kwa kutoa eneo la kuwahudumia watoto hao ili wazazi na walezi wao waweze kufanya shughuli za kujitafutia riziki.

Alitoa wito kwa wazazi na walezi kujitokeza na kuwaleta wato wenye matatizo kama hayo ili waweze kuhudumiwa. Anasema pasipo hawa watoto tusingepata fursa ya kumtumikia Mungu ambayo ni Baraka hivyo tutumike kwa moyo na upendo.

Kituo hicho kipya kipo Umoja hosteli lilipokuwa Kanisa Kuu la zamani la Moshi Mjini ambalo kwa sasa linatazamana na stendi ya mabasi Moshi Mjini.

Naye Mratibu wa BCC Mdiakonia Elirehema Kaaya katika risala yake alisema kituo hicho cha Moshi mjini kina jumla ya watoto10 na kufanya jumla ya vitu 10. Anasema kwa sasa wanawahudumia jumla ya watoto 212 katika sharika 8 za manispa ya Moshi.

Bulding a Caring Community BCC ni huduma inayoshughulika na watoto wenye ulemavu wa akili inayoshughulika na watoto waliopo nyumbani  na wale waliopo kwenye vituo katika sharika 8 za manispaa ya Moshi. Katika sharika hizo kuna vituo ambayo vinawatunza watoto hao kuanzia asubuhi hadi jioni wanaporudi nyumbani.

BCC ilianzishwa kutoa huduma hiyo kwa lengo la kuwasaidia katika matibabu, mazoezi ya mwili na pia kuwasaidia wazazi waweze kupata muda wa kufanya shughuli kutokana na kushindwa kufanya kazi wakiwa wanawahudumia watoto wao.

Picha ya pamoja baada ya Ufunguzi wa kituo cha Usharika wa Moshi Mjini cha kuhudumia watoto wenye ulemavu wa akili Septemba 6, 2022