WASIFU WA HAYATI ASKOFU DKT. ERASTO KWEKA

Dkt. Kweka aliitwa mbinguni akiwa na umri wa miaka 89.

Wasifu

Askofu Dkt. Kweka alikuwa ni mtu mwenye kipawa cha uongozi tangu akiwa shule ya msingi. Alikuwa kiranja wa wanafunzi, kapteni wa timu ya mpira wa miguu na pia kiongozi katika bendi ya shule, ambayo ilitumbuiza katika siku kubwa ya Wachagga ya kumtunuku Mangi Mkuu.

Askofu Dkt. Kweka alionyesha umahiri mkubwa katika uongozi wa Kanisa na alitoa mchango mkubwa kwa jamii kulikomfanya atunukiwe shahada mbili za Udaktari wa Heshima (Shahada za Uzamivu) “Honoris Causa” kama ifuatavyo:

  • Tarehe 26 Septemba, 1982 alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Luther Northwestern Theological Seminary cha Minnesota, Marekani, na
  • Tarehe 21 Aprili, 2002, alitunukiwa na Chuo cha Midland Lutheran College, Fremont,  Nebraska.

Baba yake alipofariki, mwaka 1948, yeye alikuwa na umri wa miaka 14 jambo lililomsababisha kubeba majukumu ya kutunza familia iliyokuwa na Mama mzazi, Babu na Bibi pamoja na ndugu zake saba. Akiwa mvulana wa umri mdogo yeye pamoja na wavulana wengine, walianzisha biashara ndogo ya kuuza matunda na mayai ya kuchemsha katika kambi za jeshi zilizokuwapo eneo la Mailisita, Weruweru, kwa lengo la kujipatia kipato.

Akiwa Mwalimu alianzisha duka nyumbani kwa lengo la kujipatia kipato. Akiwa masomoni Makumira na Marekani alianzisha bustani ya mbogamboga alizoziuza na kujiongezea kipato cha kutunza familia. Tabia yake ya kufanya shughuli za kujiongezea kipato na kujitegemea aliendelea nayo katika maisha yake yote ya utumishi na hata baada ya kustaafu. Tabia hii ya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea aliisisitiza kwa jamii na kwa wachungaji. Katika uongozi wake aliitenga siku ya Jumatatu kwa wachungaji ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ya kiuchumi na uzalishaji katika familia ili kuongeza kipato chao na kujitegemea.

Askofu Dkt. Kweka alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti kwenye ukweli hata kama msimamo huo ungetishia usalama wake.

Askofu Dkt. Kweka, alikuwa mtu mwenye kupenda amani na msuluhishi wa migogoro mbalimbali. Alikuwa ni mtu mwenye upendo, mwenye kujali na mwepesi kusamehe. Alikuwa ni baba aliyeipenda sana familia yake na kuitunza.

Askofu Dkt. Kweka alipenda sana kusoma vitabu mbalimbali, kutunza kumbukumbu na kuandika. Siku za mwisho za uhai wake alikabidhi uongozi wa Dayosisi kitabu alichoandika kinachoeleza kuhusu “Historia ya Vituo vya Dayosisi” na hii itabaki kuwa hazina kubwa kwa Dayosisi na vizazi vijavyo.

Shukrani

Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya mtumishi wake Baba Askofu Dkt. Erasto N. Kweka.

Tunaishukuru familia yake hususan mkewe na watoto kwa kumsaidia katika utumishi wake katika Dayosisi, Kanisa na jamii kwa ujumla.

Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wengi waliohusika kwa namna moja ama nyingine kumhudumia katika hali ya ugonjwa.

Tunaushukuru uongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa upendo na undugu wa Kikristo kumhudumia kiroho na kimwili akiwa Hospitali ya Muhimbili – Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kuifariji familia tangu kifo kilipotokea na kuratibu Ibada ya kuuaga mwili wake Kanisa Kuu, Azania Front pamoja na kuusindikiza mwili wake kuja Moshi.

Tunawashukuru viongozi wa Kanisa, jamii na watu wote walioshirikiana na familia na Dayosisi katika kuuguza, faraja wakati wote wa msiba, na siku ya leo kumlaza Baba Askofu.

“Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake….” ( Mdo. 13:36a)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *