Jubilii miaka 25 Agape, 40 wahitimu kidato cha 6, Chapel yazinduliwa

Shule ya Agape Junior Seminary ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini imeadhimisha Jubilii ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Jubilii hiyo imeambatana na uzinduzi wa nyumba ya wanafunzi ya kuabudia (Chapel) na mahafali ya 20 ya wanafunzi wa kidato cha 6.

Matendo hayo matatu yaliongozwa na Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo akisaidiana na Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Mch. Calvin Coola, Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mch. Javason Mrema na Mkuu wa Agape Junior Seminary Mch. Godrick Lymo.

Kabla ya Kuwatunuku vyeti wahitimu hao, Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliwaasa wanajamii kuwarithisha watoto Elimu iliyo bora yenye mafundisho ya kumcha Mungu kukuza kizazi chenye maadili mazuri.

“Ili kukuza kizazi chenye watu wenye manufaa kwa jamii ni lazima kuhakikisha watoto wanapata elimu bora itakayowapa maarifa na kumcha Mungu.”Alisema Dkt. Shoo

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 40 walitunukiwa vyeti na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo.

Aidha katika mahubiri yaliyotolewa na Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mchungaji Javason Mrema, aliwataka vijana kufanya kazi kwa bidii na kutumia ipasavyo vipawa na karama walizopewa na Mungu ili kuacha alama na kumbukumbu nzuri kwa vizazi vijavyo.

Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo akiwatunuku vyeti wahitimu wa kidato cha 6 wa Agape Junior Seminary Mei 28, 2022