Jubilii ya miaka 50 ya pembe tatu yaadhimishwa TPC, Mkataba mpya Wasainiwa

Jubilii ya miaka 50 ya uhusiano wa pembe tatu baina ya Sharika za kanda ya tano Jimbo la Kilimanjaro Kati na Sharika 3 za kanisa la Ujerumani ilifanyika katika Usharika wa TPC wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Agosti 29, 2021 katika Ibada iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini na Mwenyekiti wa Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Dkt.Fredrick Onael Shoo.

Katika Ibada hiyo Baba Askofu Dkt.Fredrick Shoo alizindua mnara wa Jubilii ya Miaka 50 uhusiano huo ambapo neno kuu la Jubilii hiyo lilitoka katika kitabu cha zaburi ya 25 14 Siri ya Bwana iko kwa wamchao, Naye atawajulisha agano lake…

Akihubiri katika Ibada hiyo Baba Askofu Dkt. Shoo alipongeza mahusiano hayo kwa kudumu kwa takribani miaka 501(971-2021) na kueleza kuwa, yamekuwa ya baraka na mafanikio makubwa katika kazi ya kueneza Injili ya Yesu Kristo.

“Nawapongeza kwa uhusiano wenu huu ambao umekuwa wa mafanikio makubwa, uhusiano huu ulianza na misioni ya Arusha Chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini na ndugu zetu wa Usharika wa, Marienwender Hanover, Saint Mary Leipzig na Stotteritz wakati huo misioni ya Arusha Chini ikiwa na washarika 500 na sasa wameongezeka na kufikia elfu 10. Kwa sasa iliyokuwa Misioni ya Arusha Chini imekuwa na ina sharika 5 hii inaonyesha kazi ya Bwana imeendelea kukua “Alisema Dkt.Shoo na kutoa pongezi.

Amesema kama neno Kuu linavyosema Siri ya Bwana iko kwao Wamchao, siri ya uhusiano huu iko kwa Yesu Kristo kupitia upendo wake Mungu usio na ubaguzi kwa wanadamu wote.

Amesema kama neon la Mungu linavyotuasa kuwa na upendo kwa watu wote, hata kwa adui zetu kama Yesu anavyotuambia tuwapende watu  wote ndiyo msingi wa mahusiano yetu ambayo yamedumu kwa miaka 50 bila kujali rangi, utaifa kwa kutizama upendo wa Mungu kwetu hata akamtoa Mwanae wa pekee Yesu Kristo akafa msalabani kwa watu wote wapate kuokolewa.

Baba Askofu Shoo aliwaasa washarika na Jamii kupendana na kuacha kulipizana visasi hata pale adui yako anapokuuz “Mtume Paulo anatuasa tusishughulike na mambo ya Kisasi na badala yake tuwaombee, Mtume Paulo katika Warumi 12:14 anasema,  wabarikini wanaowaudhi, barikini wala msilaani”Alifundisha Askofu Shoo.

Alihitimisha kwa kuhimiza kudumisha upendo kwa watu wote  na kuwaombea adui zetu ili upendo wa Mungu uwaguse mioyo yao wapate kubadilika na kuwa watu wa Mungu.

Mkataba mpya wasainiwa

Katika hatua nyingine washirika hao walisaini mkataba mpya wa makubaliano ya kuendeleza ufadhili wa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa watakaofaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika sharika 5 za Arusha Chini/Chemchem.

Wakili David Shilatu akisaini Mkataba mpya wa Elimu wa Miaka 3 baina ya pande mbili za mahusiano

Akitoa salamu za uhusiano mwenyekiti wa Uhusianon Arusha Chini/Chem chem wakili David Shilatu amesema, uhusiano wao umekuwa wa manufaa makubwa  kwa Kanisa na jamii  ambapo amesema mwaka 2018 walianzisha mpango wa ‘Scholarship program’ wa kusomesha watoto  wa kanda hiyo.

Amesema katika maadhimisho hayo wataweka sahihi ya makubaliano mengine ya miaka 3 ya kuendelea kusomesha vijana wa kanda ya tano kupitia mpango wa ‘scholarship’.

Uhusiano wa Pembe tatu

Uhusiano wa pembe tatu baina ya Hanover-Marienwerder na Leipzig- Stotteritz kwa upande wa Ujerumani  na Arusha Chini ChemChem wa kanda ya tano ya jimbo la Kilimanjaro Kati, ulianza miaka ya 1970/71 baada ya Mch. Dkt.  Wolfgang Gunter alipojiwa na wazo la kuanzisha uhusiano wa Kiroho.

Kwa msaada wa shirika la Kiinjili la Leipzig mahusiano baina yake na Mch.Dkt.Christoph Maczewski wakati huo akiwa ni Mchungaji wa eneo la Moshi  na baada ya muda mfupi yalihamia katika eneo la kusini mwa mji wa Moshi.