Juma la Askofu na Vijana; Disemba 12-16,2022

Ni Disemba 14, 2022 siku ya pili ya Juma la Askofu na vijana, vijana wakiendelea kujifunza mada mbalimmbali.  Mch. Fadhili Lyamuya  kutoka Usharika wa Kashashi anafundisha mada kuhusu  Urafiki Uchumba hadi Ndoa.

Katika mada yake anafafanua maana ya urafiki Kibiblia. Anasema katika urafiki Biblia inasema unapaswa kumpenda rafiki yako kama nafsi yako akitolea mfano wa Yonathan alivyompenda Daudi hata kujitoa kwa ajili ya usalama wake. 1 Samweli 18:1-4.

Anasema Yonathan mwana wa mfalme Sauli alionyesha upendo kwa Daudi bila kujali yeye kama mzaliwa wa kwanza anaweza kupoteza nafasi yake ya kiti cha ufalme dhidi ya Daudi hata uhai wake pia.

Mch. Lyamuya anasema urafiki ni matokeo ya kutambuana na kuthaminiana, mtu anapokosa kupendwa au kuthaminiwa na kutambulilika anajisikia kukosa thamani, upendo na  kusababisha kuugua hata sonona.

“Mtu ameumbiwa upendo, thamani na utambulisho; tunahitaji marafiki kwa sababu ya kujaza hitaji la kibinadamu la kushirikiana, kusaidiana na kuchangamana”. Alisema Mch. Lyamuya

Anasema binadamu hajaumbiwa kujitosheleza peke yake, ili kujitosheleza unahitaji kutoshelezwa na mtu mwingine ambaye ni rafiki yako.

“Tunahitajiana, huwezi kujua wala kufanya kila kitu mwenyewe katika maisha, hivyo unahitaji rafiki wa kushirikiana naye, tunahitaji marafiki ili tuweze kujifahamu tulivyo, na mtu kujifahamu ni lazima awepo atakayekwambia, rafiki pekee ndiye anaweza kukwambia unahasira, ni mpole, una mwanya, n.k.”Alisema Mch. Lyamuya

Alitaja aina za marafiki kuwa  ni pamoja na marafiki wa mbali tunaokutana nao na kushirikiana nao katika mambo mbalimbali. Pia alisema wapo marafiki wa kawaida, ambao tunakua nao kwa sababu ya kupenda kufanya vitu vinavyofanana, mfano kuimba,  kupiga gitaa nk.

Ansema pia kuna marafiki wa karibu, hawa wanapenda kushirikishana mambo muhimu hata mambo ya siri pia. Vile vile altaja marafiki walezi. Anasema marafiki hawa huwa wametutangulia umri, uzoefu, maarifa ya kimaisha na kiroho. Anasema kwa vijana ni muhimu na ni lazima kuwa na marafiki kama hawa kwa ajili ya malezi. “Ujuzi katika kazi, masomo, mahusiano, unahitaji kuwa na rafiki mlezi”Alikaza Mch. Lyamuya.

Katika dhana ya rafiki akielekea kwenye mjumuisho wa mada ya rafiki, uchumba hadi ndoa; alisema aina hii ya urafiki  ni ile ya  rafiki wa moyoni. Huyu ni rafiki ambaye ni mmoja tuu, uliyempa nafasi ya pekee katika moyo. Ni rafiki mpenzi, mchumba mpenzi mume mpenzi na mke mpenzi

Sifa ya aina ya huyu rafiki ni anayekufahamu vizuri na unayemfahamu vizuri; majina, historia, ndugu, matakwa yenu n.k.

Pia ni rafiki anayependa kuwa nawewe, anayejisikia vibaya unapokuwa mbali nawewe, anayependa kuwasiliana nawewe. “Mawasiliano hudumisha mahusiano, kama hakuna mawasiliano baina yenu ujue hakuna mahusiano”Anasema Lyamuya. Mch. Lyamuya anataadharisha urafiki huu usijengwe kwenye misingi ya kuthamini zawadi na ahadi zisizotekelezeka (Mali).

Anahitimisha kwa kusistiza kuwa mahusiano yajengwe katika misingia ya kweli na kuaminiana na sii kwa kudanganyana kuwa na ndoa zinazodumu na zisizo na mafarakano.

Mada nyingine iliyofundishwa ni kuhusu ufugaji wa kisasa wa kuku pamoja  kilimo cha umwagiliaji kwa njia matone iliyowasilishwa na Bw. Erasto Mbele kutoka Norwegian Church Aid (NCA)

Mch. Fadhili Lyamuya akifundisha mada inayohusu urafiki, uchumba hadi ndoa.