Kidia: Usharika wa Kidia wakabiziwa zahanati Kuiendesha

Usharika wa Kidia wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, umekabidhiwa rasmi Zahanati ya Kidia kuiendesha kufuatia ombi la Usharika huo kwa Dayosisi na ombi lao kukubaliwa katika kikao cha 244 cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini.

Makabidhiano hayo yalifanywa  na Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mch. Javason Mrema ambapo Mch. wa Usharika Sayuni Shao alipokea hati ya makabidhiano kwa niaba ya Washarika wa Kidia Aprili 16, 2023.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ibada iliyoongozwa na Mkuu wa Jimbo la Kati akishirikia na na Mku wa pili wa Jimbo hilo Mch. Israel Moshi na Mch. Kiongozi wa Usharika Sayuni Shao.

Pia makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Katibu wa Afya wa Dayosisi Bw. Joshua Ndaga, Katibu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Bw. Regnald Hosea, wawakilishi wa Usharika ambao ni Mzee Kiongozi wa Usharika Bw. Allen Mmary, Ms. Eliaichi Mkonyi ambaye ni Mzee wa Usharika na Bw. Leonard Malisa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Usharika.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Kidia Sayuni Shao kwa niaba ya Washarika, aliushukuru uongozi wa Dayosisi kwa kukubali ombi lao na kulitekeleza kwa vitendo.

Aidha aliahidi kuwa, Washarika wa Kidia watawekeza nguvu zao kuhakikisha zahanati hiyo inarudisha huduma za afya na kuziboresha na hatimaye kuwa kituo cha afya cha mfano wa kuigwa katika Dayosisi.

Ibada ya Makabidhiano ya zahanati ya Kidia kwa Usharika wa Kidia kuiendesha