Kilele Wiki ya Afya Kidayosisi Chafanyika Usharika wa Masia Mamba

Kilele Wiki ya Afya Kidayosisi Chafanyika Usharika wa Masia Mamba

Msd. Ask. Mch. Msanya asema Una uhuru wa kuchagua hali yako ya afya ya kimwili na kiroho”

  • Washarika wahamasika kupima afya
  • Vyakula vya asili vyatamba
  • Mazoezi mepesi ni kinga nafuu zaidi dhidi ya magonjwa

Kwa takribani miaka arobaini na mbili (42) sasa, Dayosisi ya Kaskazini imekuwa na kaida njema ya kuandaa na kuratibu Wiki ya Afya Kidayosisi kila mwaka kupitia Idara ya Afya. Wiki hiyo inayofanyika kila mwezi Juni katika ngazi ya Sharika, Majimbo na Kilele kuadhimishwa Kidayosisi huambatana na masuala na shughuli muhimu zenye mkazo wa pekee katika kuwapa na kuwajengea uwezo Washarika kuhusu taarifa, maarifa na ujuzi wa kinga dhidi ya maradhi mbalimbali hususan yale yasiyoambukiza.

Aidha, Wiki ya Afya huwa na maudhui maalumu ya mwaka husika yanayojengwa katika mstari maalumu kutoka Biblia. Mwaka 2023 maudhui maalumu ni “Kuwa na Kiasi” na yalijengwa katika Mithali 23:2.

Tena ujitie kisu kooni kama ukiwa mlafi;”

 Aghalabu, maadhimisho ya Kidayosisi huambatana na Ibada maalumu sambamba na maonesho ya shughuli mbalimbali zinazohusiana na Elimu ya Afya ya Msingi kadhalika upimaji wa afya na hufanyika katika usharika mmojawapo wa Dayosisi. Mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika Jumapili tarehe 11 Juni, katika Usharika wa Masia Mamba Jimbo la Kilimanjaro Mashariki mgeni rasmi akiwa ni Msaidizi wa Askofu Mch, Deogratius Msanya.

Akihubiri katika ibada hiyo Msd. Ask. Mch. Msanya alisema Mungu amempa mwanadamu jukumu la kutunza afya yake ya kiroho na vilevile afya ya kimwili. Na hivyo, hatima ya matokeo chanya au hasi ya afya ya kiroho na kimwili ni juu ya uchaguzi wa mtu mwenyewe alisisitiza.

Msd. Ask. Aliendelea kuhubiri akisema, “Ni jukumu la kila mmoja kufanya uchaguzi wa kuchagua afya bora ya mwili na roho na ili kuweze kufaya uchaguzi katika afya hizi mbili ni lazima kujitambua upo katika hali gani kiroho na kimwili” alisema.

Katika kufafanua zaidi, Msd. Ask., alieleza kwamba, “Kwa upande mmoja, katika afya ya roho, Roho Mtakatifu ndiye anayetusaidia kujitambua kama tupo katika njia sahihi ya Mungu na vilevile Neno la Mungu linapohubiriwa linatusadia kujitambua na kutuweka wazi kutambua kama afya zetu za kiroho zipo sawasawa na kwa upande wa pili katika afya ya miili yetu ni pindi tunapopima afya zetu mara kwa mara kwa wataalamu wa afya ndipo tunajitambua hali zetu kiafya na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu afya zetu mkazo mkubwa zaidi ukiwa ile kaulimbiu maarufu ya kinga ni bora kuliko tiba.”

Pia alisisitiza kwa kusema, “Endapo hauendi kanisani mahali Neno la Mungu linapohubiriwa huwezi kufahamu afya yako ya kiroho, pia usipokwenda hospitali kwa wataalamu wa afya kupima huwezi kufahamu afya ya mwili wako.”

Akihimiza Neno Kuu kutoka Mit. 23:2, Msd. Ask. aliwachagiza Washarika kuzingatia aina ya vyakula wanavyokula na madhara yake katika miili. Alitahadharisha kwamba, kuendekeza tamaa za mwili bila kuzingatia tunakula nini, kwa kiasi gani na kwa wakati gani ni bayana tutaishia kuharibu afya za miili yetu. Aidha, aliwaasa Washarika na jamii kwa ujumla kutokudharau vyakula vya asili k.v. vibere, viazi vikuu, ngararumu n.k alihitimisha Msd. Ask.

Naye mtaalamu wa Afya, Dkt. Apolnary Shao akitoa mada kuhusu ugonjwa wa Presha na Kisukari alisema ni vyema kupima na kufahamu hali ya afya yako na kuzingatia ushauri utakaopewa na wataalamu kuepuka mazara na gharama kubwa za matibabu hali ya ugonjwa inapokuwa kubwa.

Mada hii iliwasisimua wasikizaji nakujtokeza kwa wingi kupima afya zao.

Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Bibi. Norah Robart (wapili kushoto) ambaye ni Mratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi jimbo la K/Mashariki kwenye banda la vyakula vya asili siku ya Kilele cha wiki ya Afya Kidayosisi Usharika wa Masia Mamba Juni 11, 2023