KITABU ‘KYA FIIBO NA MIIDILE YA KISIHA’ CHAZINDULIWA

Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Mhe. Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amezindua na kuweka wakfu Kitabu Kipya cha Nyimbo na Liturgia kwa lugha ya Kisiha (Fiibo na Miidile ya Kisiha) katika Usharika wa Sanya Juu Jimbo la Siha tarehe 6 Agosti 2021.

Amelipongeza Jimbo la Siha kwa kupatikana Kitabu hicho akisema, “Hakuna kitu kitamu kama lugha ya Mama.” Na kunukuu ushairi wa Shaaban Robert usemao, “Titi la mama ni tamu, linatia hamu hata kama ni la mbwa.”

Akihubiri toka Kitabu cha Mithali 3:5-7 amewataka washarika kuenenda kwa hekima kwa njia ya kumtumaini BWANA, kumkiri BWANA, kumcha BWANA na kuchukia Uovu.

Lengo la kuzindua Kitabu hicho ni kuwaita na kuwafundisha watu kumcha BWANA kwa kuimba kwa lugha yenye mguso, lugha ya mama. Lugha ya mama ikipotea huo utakuwa ni umasikini Mkubwa.

Mkuu wa Jimbo la Siha, Mch. Elisa Kileo, amesema Kitabu kya Fiibo na Miidile ya Kisiha kimeandaliwa toka 2005 wakati wa Mkuu wa Jimbo Mch. Eligurd V. Nasari.

Askofu Dkt. F. Shoo akikata utepe kuzindua kitabu cha Nyimbo na Liturugia cha lugha ya Kisiha Agosti 6, 2021.