MAADHIMISHO YA SIKU YA CCT

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeiomba serikali kuangalia suala la kodi kwa taasisi za dini zinazotoa huduma za Afya na elimu, kwani imekuwa changamoto na kupelekea Taasisi hizo kutoa huduma kwa kusuasua.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Fredrick Shoo amesema kilio cha kodi kwa taasisi hizo ni kikubwa na endapo hilo halitaangaliwa, litasababisha baadhi ya taasisi kujifunga kwa kushindwa kujiendesha.

Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya CCT, ambapo yamefanyika kitaifa katika usharika wa Moshi mjini mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, akiwemo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

“Mambo ya kodi yanatuumiza sana taasisi za kanisa, yaani tunapigwa kodi nyingi tunafikia mahali ambapo tunaonekana washindani au kama maadui na nyingine zimefikia mahali ikiendelea hivyo itajifunga kutokana na kushindwa kujiendesha,” amesema Dk Shoo.

Ameongeza kuwa, “Leo Serikali kama imejiweza kujenga zahanati zake, vituo vya afya na shule, ambapo najua bado haijatosha, lakini isije ikawa ni sababu ya kupigana, yaani kuja na kodi hizi ambazo unajua kabisa kituo kikilipa hakika ni kama unataka kufunga kile kituo, naomba hekima itumike,” amesema.

“Nasema mambo haya hayapo sawa waziri na hii haitakuwa baraka kwa nchi hii tukijua taasisi hizi, zinamuhudumia na zinasaidia katika kuongeza huduma kwa watanzania, kilio ni kikubwa, mkayafanyie kazi hili kwa baraka kwa manufaa ya nchi hii ya Tanzania,” amesema.

Aidha Dk Shoo ametumia pia nafasi hiyo kuiomba serikali, kuendelea kulitazama suala la kodi kwenye taulo za kike (Sodo) ili kuwezesha upatikanaji wake kwa urahisi na kuondoa changamoto ambazo hupitia watoto wa kike wanapokuwa kwenye hedhi.

“Ndugu waziri najua kuna hatua zimechukuliwa na serikali katika suala hili la taulo za kike, lakini naomba iendelee kuangalia jambo la kodi kwenye hili, Watoto wasije wakapata maambukizi kwa sababu ya kutumia matambara na vitu vingine ambavyo havitunzi afya zao”

Dk. Shoo amewataka pia wazazi na walezi kulitazama suala hilo, na kuhakikisha watoto wanapoomba fedha kwa ajili ya kununua taulo hizo wanahudumiwa, ili kuweza kuwa na hedhi salama.

Akitoa taarifa Katibu Mkuu wa CCT Dk. Canon Matonya amesema jumuiya hiyo inafanya shughuli mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za serikali ambapo makanisa wanachama yanamiliki taasisi zinazotoa huduma za afya 219 na taasisi za elimu 255.

Amesema pamoja na jitihada hizo changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwapa ugumu katika kutoa huduma kwenye taasisi hizo ni kudaiwa kodi za mapato kutokana na huduma za afya na elimu wanazozitoa.

“Taasisi zetu nyingi za kanisa zinakabiliwa na changamoto ya kudaiwa kodi za mapato kutokana na huduma za afya na elimu zinazotolewa,TRA wamekuwa na mtazamo kuwa taasisi hizi zimekuwa zikiingiza faida kutokana na huduma hizo, tunaomba serikali itazame hili na kuondoa kodi hizo ili kuzisaidia taasisi kuendelea kutoa huduma”.

Mbali na hilo, aliishauri serikali kufanya marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu sekta binafsi ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko.

“Tunaishauri serikali kuimarisha sekta binafsi kwa kuhamasisha watu kutoka ndani na nje ya nchi yetu kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha mashamba makubwa ya mazao ya chakula na biashara, lakini pia wawekezaji binafsi wahamasishwe zaidi kujenga viwanda vya kusindika mazao ya ndani ya nchi”

“ Serikali ifungue masoko ya uhakika ya wakulima wadogo wadogo, lakini pia tunashauri marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu sekta binafsi yafanyike ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko”.

Waziri wa Fedha na mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema amepokea kwa niaba ya serikali maombi na ushauri uliotolewa na kwamba suala la kodi kwa taasisi za dini, serikali imeendelea kulifanyia kazi na itatoa taarifa wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024.