Mch. Llamweeki Ndosa Astaafu kwa Heshima, Alitumikia Kanisa Miaka 32

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. Llamweeki Ndemfoo Ndosa Januari 29, 2023 katika Usharika wa Ng’uni Jimbo la Hai.Baba Askofu Dkt. Shoo aliongoza ibada hiyo akishirikiana na Askofu Scott Johnson wa Synod ya Nebraska, Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Mallyo, Mkuu wa pili wa Jimbo la Hai Mch. Dominic Mushi, Mch. Kiongozi wa Usharika Christian Kweka na Mch. mwenza Leonard Minja.Akitoa salamu zake, Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, alimshukuru Mungu kwa huduma ya Mch. Llamweeki Ndosa katika kulitumikia Kanisa la Mungu na jamii. Anasema Mchungaji Ndosa amekuwa mmoja wa wachungaji wa mfano katika Dayosisi kwa jinsi alivyoifanya kazi yake kwa bidii na uaminifu.“Mchungaji amekuwa wa baraka na wa mfano wa kuigwa, alifanya kazi yake bila ulegevu wala kujali ni wapi ulipopangwa kuifanya kazi ya Mungu. ” Alisema Askofu Dkt. ShooAlisema Mch. Ndosa alikuwa mtunzaji mzuri wa Mazingira na alizingatia sana azimio la Dayosisi la kila Mwanafunzi wa Kipaimara anapoanza kuotesha miti kumi na kuitunza kabla ya kupata kipaimara.Aidha Baba Askofu Dkt. Shoo alitoa wito kwa jamii yote kuhakikisha wanajihusisha katika kutunza mazingira yanayowazunguka ikiwa ni pamoja na kupanda miti katika maeneo yao na kutunza vyanzo vya maji.“Nitoe wito kwamba kila mmoja wetu aone anawajibu wa kulinda na kuhifadhi mazingira; Ukosefu wa mvua, ukame wa ajabu mafuriko ni matokeo ya sisi kucheza na uumbaji wa Mungu. Niombe kila mmoja kwa nafasi yake aendeleze jitihada za kuotesha miti, kutunza vyanzo vya maji na kufanya kila jitihada kulinda na kutunza mazingira yetu.”Alisema Askofu Dkt. Shoo.Naye Askofu Scott Johnson wa Synod ya Nebraska alimpongeza Mch. Ndosa kwa kazi yake nzuri kama mchungaji katiaka shamba la Bwana. Mch. Llamweeki Ndosa ametumika katika huduma ya kichungaji kwa miaka 32 na serekalini kama afisa misitu kwa miaka 4. Akisoma wasifu wa Mchungaji Ndosa, Katibu Mkuu Msaidizi na Mtunzahazina wa Dayosisi ya Kaskazini CPA Munguatosha Makyao alisema, Mch. alisoma stashahada ya Theologia katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mwaka 1985-1989 na Shahada ya Theologia ya Chuo Kikuu cha Makumira (1998-2001).CPA Makyao alisema baada ya kuhitimu stashahada ya Thelogia mwaka 1989, alibarikiwa kuwa Mchungaji katika Usharika wa Mafeeto mwaka 1989.Alitumika kama mchungaji kiongozi katika sharika za Sanya Juu (1990-1994), Siha (1995-1998), Kawaya (2001-2003), Roo (2004-2006) na mwaka 2007 hadi alipostaafu Januari 29, 2023 alitumika katika Usharika wa Ng’uni.

Askofu Scott Johnson wa Nebraska akihubiri katika ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. Ndosa katika Usharika wa Ng’uni, Januari 29, 2023