Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya Saria (Mstaafu), amesema hatupaswi kuwapuuza wanawake kwani wanawake wanamchango mkubwa katika jamii. Mch. Saria aliyasema hayo katika ibada ya siku ya kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo katika Usharika wa Sembeti Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Machi 31, 2024.
Akizungumza katika salam zake za Pasaka, alisesema wanawake wasipuuzwe kwani wana umuhimu katika jamii, hata mtu wa kwanza kumwona Yesu baada ya kufufuka na kutoka kaburini alikuwa ni mwanamke.
Alisema kama tulivyoona ujasiri wa mwanamke katika biblia, ni wito wangu kwa wanawake kusheherekea Pasaka kwa vitendo, mnapaswa kuishi maisha matakatifu mkimlilia Mungu, na mkilia kwa ajili ya watoto wenu ili Mungu awasaidie na kuwarejesha katika maadili na mienendo inayompendeza Mungu.
Aliongeza kuwa, Yesu alifufuka na kuishi katika maisha yetu akitolea mfano wa Paulo, Petro na Sila. Katika hili Yesu analithibitisha Neno lake katika familia zinazomwamini na kumtegemea.
Katika hatua nyingine Mch. wa Usharika wa Sembeti Richard Njau aliwaonyesha Msaidizi wa Askofu Mch. Elingaya Saria na pamoja na wageni waliohudhuria ibada hiyo jengo na mashine ya Kusaga na kukoboa pamoja na mashine ya kuranda mbao. Mch. Njau aliwashukuru washarika wa Sembeti kwa kazi kubwa waliyoendelea kufanya katika ujenzi huo.
Pia alimshukuru Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi kwa washarika wa Sembeti waliopo Dar Es Salama Kanali Richard Moshi kwa jitihada kubwa alivyoifanya katika kuhakikisha ujenzi wa mashine hizo unakwenda vizuri na kumwomba afikishe salam hizo kwa Washarika hao. Mch. Njau alisema mashine hiyo imekuwa msaada na baraka kubwa kwa wanakijiji wa Sembeti na kwa sasa mashine hiyo inatoa huduma katika eneo hilo kwa bei nafuu. “Debe moja tunasaga kwa shilingi mia tatu badala ya shilingi mia nne hadi miatano katika maeneo mengine”.
Alihitimisha kwa kueleza kuwa, kwa sasa wanaweka jitihada kubwa katika kumalizia jengo hilo la mashine kabla ya kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Dayosisi Askofu Dkt. Fredrick Shoo mapema mwaka huu.
Pia katika Ibada hiyo Msaidizi wa Askofu mstaafu Mch. Elingaya Saria aliwaingiza kazini wazee wa Baraza la Usharika, kamati ya jengo pamoja na kumuaga mzee mmoja wa Baraza la Usharika ndugu Sauli Temu aliyemaliza kipindi chake.