Mhandisi Z.S. Moshi: Ni muhimu kwa kiongozi kuwa na sifa za Kiongozi na sifa za Mtawala

Hayo yalisemwa na Mhandisi Z.S. Moshi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini alipokuwa akiwasilisha mada ya Uongozi na Utawala katika semina kwa wanafunzi wa kozi ya Ushauri na Utunzaji wa Kichungaji katika Chuo cha  Ushauri na Utunzaji wa Kichungaji (CPE) ndani ya hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) iliyoko chini ya chama cha Msamaria mwema mnamo siku ya Jumatano tarehe 14 Juni, 2023.

Akieleza kuhusu umuhimu wa uongozi, mifumo ya utawala na utendaji, namna ya kupunguza changamoto na mambo muhimu ya kuzingatia kuongoza kwa ufanisi. Mhandisi Moshi alikazia suala la kuweka mipango katika taasisi au kituo akisema, “mipango ni jambo muhimu na lazima kwa sababu mipango inatupa malengo, inatuunganishia njia ya kufikia malengo, inaweka wajibu wa watumishi na vilevile inatupa misingi ya uwajibikaji.”

Kuhusu uongozi na utawala,  Mhandisi Moshi alisema, “kiongozi anapaswa kuwa  mtu mwenye kutenda haki wakati wote, mwenye msimamo wa kusimamia taratibu na sharia na mwenye uwezo wa kujifunza tabia, vipawa na uwezo wa wafanyakazi wake.” Aliendelea kusisitiza kwamba, “kiongozi ni lazima awe ni mtu mwenye maono kwa Kiingereza a Visionary leader, jasiri na anayejitoa kwa wafuasi wake, anayeaminika kwa Kiingereza Trustworthy na vilevile awe mwenye ufahamu na uelewa wa kutosha kwa Kiingereza knowlegeable and understanding.”

Kuhusu mtawala, Mhandisi Moshi alisema kwamba, “mtawala ni mtu mwenye ujuzi maalumu na wajibu wa kusimamia kikundi kwa kutumia sheria na taratibu. Pia ni mtu anayezingatia malengo, anasimamia usahihi kwenye utendaji, anasimamia utekelezajia wa mpango wa taasisi na anawawajibisha wanaokiuka utaratibu.” Mhandisi Moshi alihitimisha mada hiyo kwa kusisitiza kwamba, ni muhimu kiongozi yeyeote wa Taasisi ama kikundi awe na maarifa, taarifa na ujuzi katika Uongozi na Utawala kwa uwiano sawa ili kuleta ufanisi na tija.

Kozi ya Ushauri na Utanziji wa Kichungaji kwa Kiingereza Clinical Pastoral Education (CPE) hutolewa kwa wanafunzi/ wahitimu wa mafunzo ya thiolojia hususan Wachungaji na pia kwa wahudumu wa imani na madhehebu mengine k.v. mapadri, maimamu, mitume n.k. kozi hii huwajengea uwezo na kuwapa wahitimu stadi za kutosha za kuwaendea, kukutana na kuwasaidia watu waliopitia uzoefu wa hali au changamoto ngumu katika maisha zilizo ama zinazoleta maumivu ya hisia kwa Kiingereza trauma.

Wanafunzi wa CPE katika semina ya Uongozi na Utawala Bora iliyofanyika katika chuo cha Ushauri na Utunzaji wa Kichyngaji KCMC jUNI 14, 2023