Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ameongoza ibada ya harambee ya ujenzi wa kanisa pamoja na shukrani ya familia ya Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro katika usharika wa Kondeni Matala Aprili 23, 2023.
Harambee hiyo iliongozwa na Mch.Eliona Kimaro wa Usharika wa Kijitonyama KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambapo Usharika wa Kondeni Matala ndio Usharika wake wa nyumbani.
Katika harambee hiyo, jumla ya Shilingi milioni 425 zilikusanywa ambapo pesa taslimu zilizotolewa hapohapo ni shilingi milioni 78. Lengo lilikuwa kukusanya shilingi milioni 400.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba, Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Molel, na Wabunge Esta Bulaya na Halima Mdee wa viti maalumu, Priscus Tarimo wa Moshi Mjini, Dkt. Mathayo David Mathayo wa Same Magharibi, Festo Sanga wa Makete, Dkt. Charles Kimei wa Vunjo na Mbunge wa Kibaha Silvesta Fransisi Koka.
Akihubiri katika Ibada hiyo, Baba Askofu Dkt. Shoo aliwataka viongozi kuwa waadilifu na kutumika kwa uaminifu badala ya kutumia nafasi zao kujitajirisha.
Alisema ni hali mbaya kwa taifa ikiwa viongozi wa kisiasa wanatumia nafasi zao vibaya kujitajirisha badala ya kusimamia miradi ya maendeleo ya taifa.
“Viongozi mjue kuwa kujali maslahi binafsi na kuwaonea wanyonge ni jambo linalomchukiza Mungu na linasababisha taifa kuingia katika shida. Taifa la Walawi liliingia katika adhabu kwa sababu ya viongozi wa taifa kutokusimama ipasavyo katika nafasi zao”Alisema
Aidha aliwataka wachungaji, na watumishi wa kiroho kuacha kuwababaisha watu kwa kuwalaghai ili kujipatia fedha na utajiri. “Kwa taifa letu tunahitaji viongozi wa kiroho watakaosimamia maadili, watakao watunza watoto katika kumjua Mungu na sio wale wanaojali maslahi yao binafsi” Alisema Askofu Dkt. Shoo