Mkutano Mkuu K/Mashariki, Askofu Dkt. Shoo: Tusimame na Yesu Katika Changamoto

Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo Mwenyekiti wa CCT ambaye ndiye Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini amewataka Wakristo na jamii kwa ujumla kusimama na Yesu wakati wote hasa wakati jamii inapopita katika changamoto mbalimbali likiwemo janga la Uviko 19.

Askofu Shoo amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Jimbo la Kilimanjaro Mashari la KKKT Dayosisi ya Kaskazini uliofanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Biblia  na Theolojia Mwika Agosti 8, 2021.

Askofu Dkt. Shoo amesema taifa na Jamii limepita katika wakati Mgumu lakini Mungu amekuwa akitupigania wakati wote, “Pamoja na kupita katika changamoto za kiuchumi, siasa na janga la Korona lakini bado tumeweza kufanya kazi nyingi na kubaki salama, hili limenifanya ni zidi kuamini kuwa kwa Mungu hakuna wakati Mgumu na wakati wote anatupigania.”alisema Dkt. Shoo

Aliitaka jamii kuendelea kumwomba Mungu na kumtegemea wakimsikiliza roho mtakatifu kwa kila jambo wanalofanya kwa maendeleo ya Kanisa na jamii.

Amewapongeza jimbo la Kilimanjaro Mashariki kwa kazi mbalimbali walizofanya jimboni hapo na kushiriki kwao katika kazi za Umoja katika Kanisa.

Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ndiye Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Mchungaji Calvin Koola akiwasilisha taarifa yake, alimshukuru Mungu kwa kuwalinda katika Mikono yake hodari kiasi ambacho wameweza kutekeleza majuku yao vizuri.

Amesema pamoja na changamoto za Kiimani, kiuchumi, kijamii na kiafya hususani katika kipindi cha janga la Uviko 19, wameweza kutekeleza majukumu yao kwa kadiri Mungu alivyowajalia.

Aliwataka wajumbe wa Mkutano huo, washarika na jamii kwa ujumla kuzingatia tahadhari zote za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19 bila kusahau magonjwa mengine yanayosababishwa na mifumo ya Maisha, uharibifu wa mazingira na mambo mengine.

Mkutano huo  uliofunguliwa na Askofu Dkt. Fredrick Shoo hufanyika kila baada ya miaka miwili ambao huamua mambo ya msingi kuhusu mipango  na mstakabali wa Jimbo, Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.

Neno Kuu la mkutano lilitoka katika kitabu cha Mathayo 19:17 “Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi”?

Askofu Dkt. Fredrick Shoo wa 4 kushoto, Msaidizi wa Askofu wa 4 kulia, Mkuu wa jimbo la Kilimanjaro Mashariki wa 3 Kushoto, msaidizi wa Askofu mstaafu wa 2 Kulia kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki KKKT Dayosisi ya Kaskazini.