Mkutano Mkuu wa 42 wa Elimu ya Afya ya Msingi wafanyika

Mhe. Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Deogratius Msanya, amefungua Mkutano Mkuu wa 42 wa Elimu ya Afya ya Msingi, machi 28, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Umoja Lutheran Hostel.

Msaidizi wa Askofu akifungua Mkutano huo alimshukuru Mungu kwa kuwalinda na wameweza kuonana tena pamoja na changamoto ya ugonjwa wa covid 19.

Vile vile, aliwashukuru waratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi kwa jinsi wanavyojituma katika kutunza afya za watu. Alisema Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchill aliwahi kusema kuwa taifa lolote haliwezi kuendelea kama halina watu wenye afya njema. Hata kanisa haliwezi kufanikiwa kama halina washarika wenye afya njema hivyo, ni muhimu sana kutunza afya kwa jamii ili kuwa na taifa na kanisa lenye maendeleo.

Alisema suala la afya ni la kipau mbele maana hata  tunapokwenda kuwahubiria watu habari njema za Mungu, kama hawana afya njema ni ngumu  kufanikiwa.

Aidha, alitoa  wito kwa wajumbe kutoa taarifa kwa wakati, ili kuweza kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa wakati na kuendelee kuboresha afya za watu wa Mungu.

Naye Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mch. Javason Mrema akiongoza sala ya ufunguzi alisema, yale yote wanayofanya kuwasaidia na kuwaelekeza watu wetu kuhusu masuala ya afya yafanyike kwa kumtegemea Mungu.

Naye Mratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi Dayosisi Sir. Isaria Megiroo akiwasilisha miniti ya kikao kilichopita alisema, kuna umuhimu wa kutazama maisha yetu hususani kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema suala la magonjwa yasiyoambukiza limeendelea kuwa tatizo kubwa miongoni mwa Washarika na jamii kwa ujumla.

“Tatizo hili linachangiwa kwa kiwango kikubwa na tabia na mwenendo wa maisha husuani katika kula, kunywa na kutokufanya mazoezi”Alisema Megiroo.

Alihitimisha kwa kuwashukuru wajumbe kwa kufika na kuwasihi kudumisha ushirikiano na mshikamano katika masuala ya Elimu ya Afya ya Msingi na upimaji wa Afya.