Mosaic International Watembelea KKKT DK Hedikota

Mosaic International Watembelea KKKT DK HedikotaUjumbe wa watumishi 11 ukiongozia na Bibi. Donna Garst kutoka Shirika la Mosaic International Marekani, umetembelea hedikota ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Februari 7, 2023, katika ziara yao ya kujifunza namna Kanisa linavyotoa huduma zake hapa nchini hasa kwa walemavu wa akili. Mosaic International ni washirika wanaofadhili watoto wenye ulemavu wa akili kwa kushirikiana na KKKT Dayosisi ya kaskazini chini ya kitengo chake cha Building a Caring Community (BCC) cha Idara ya Udiakonia.Akiwakaribisha katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Mhandisi Zebadiah Moshi alitoa ufafanuzi kuhusu Muundo wa Dayosisi na jinsi unavyofanya kazi pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Dayosisi kupitia idara na vituo vyake.Ziara yao imelenga kubadilishana uzoefu katika utoaji huduma za kijamii hususani kwa walemavu wa akili na vilevile kujifunza tamaduni mbalimbali za hapa nchini. Mratibu wa BCC Mdiakonia Elirehema Kaaya akiwasilisha taarifa yake kuhusu BCC na kazi wanazozifanya katika kuwahudumia watoto na vijana wenye ulemavu wa akili, alisema kwa sasa wanawahudumia watoto 219 katika sharika 8 za Manispaa ya Moshi. Alisema BCC ni huduma inayoshughulika na watoto wenye ulemavu wa akili waliopo nyumbani na wale waliopo kwenye vituo 10 katika sharika 8 za manispaa ya Moshi.Katika sharika hizo kuna vituo ambayo vinawatunza watoto kuanzia asubuhi hadi jioni wanaporudi nyumbani na wengine wakipatiwa huduma manyumbani kwao.Aliongeza kuwa BCC ilianzishwa kutoa huduma hiyo kwa lengo la kuwasaidia watoto katika matibabu, mazoezi ya mwili na pia kuwasaidia watoto wanapofikia umri wa ujana kuweza kujitegemea kwa kuajiriwa au kujiajiri na vilevile kuwasaidia wazazi/walezi waweze kupata muda wa kufanya shughuli zao kutokana na kushindwa kufanya hivyo kwa kuwahudumia watoto wao kutwa.

Katibu Mkuu KKKT DK, Mhandisi Zebadiah Moshi aliyesimama akiwakaribisha wageni kutoka Mosaic International Februari 7, 2023 hedikota ya DK, kulia ni Mratibu wa BCC Md. Elirehema Kaaya na kushotu ni Kiongozi wa ujumbe wa watu 11 toka Mosaic International Bibi. Donna Garst