MOSHI MJINI: KATIBU MKUU AINGIZWA KAZINI, WATHEOLOJIA WABARIKIWA

Mkuu wa Kanisa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo amemwingiza kazini Katibu Mkuu Mteule Injinia Zhebadia Moshi na kuwabariki Watheolojia wanne kuwa Wachungaji katika ibada iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini Machi 6, 2022.

Injinia Moshi aliingizwa kazini rasmi baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini katika kikao cha Halmashauri Kuu ya 241 kilichofanyia Disemba 7, 2021 Uhuru Hotel and Conference Centre.

Akihubiri katika ibada hiyo Baba Askofu Dkt. Shoo alimpongeza Injinia Moshi kwa kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini. Aidha Aliwapongeza watheolojia 4 Arnold Swai, Bernard Mushi, Godson Moshi na Nelson Shoo waliobarikiwa kuwa Wachungaji.

Baba Askofu aliwaasa kuwa katika wajibu na huduma waliyoitiwa wasimame na Yesu, wamtii na wazidi kila siku kumwomba Roho Mtakatifu kushinda majaribu. Tumtegemee Roho Mtakatifu atupe nguvu ya kuyashinda majaribu tunayokutana nayo.

Mara baada ya kuingizwa kazini Mhe. Katibu Mkuu alishukuru wote waliohudhuria na kushuhudia kuingizwa kwake kazini na kubarikiwa kwa watheolojia.


Alisema ili kufanya kazi hii kwa ufanisi anahitaji sana Roho wa Mungu kumwongoza “Naomba mniombee kuifanya kazi ya Mungu kulingana na mapenzi ya Mungu na si kwa mapenzi ya Mwanadamu” Alisema Injinia Moshi.

Alisema pale tunapofanya kazi kwa mapenzi yetu na kuacha mapenzi na mipango ya Mungu ndipo chanzo cha migogoro na mafarakano katika kazi. Anasema si mara zote hatutekelezi mapenzi ya Mungu kwa kutosikia sauti ya Mungu bali inatokea tunapokosa ujasiri wa kusimama katika mapenzi ya Mungu na kufuata mapenzi ya wanadamu.

Alisema  anaamini kama Mungu alivyowaongoza Musa na Joshua wakatimiza mapenzi ya Mungu na kufika katika nchi ya ahadi hivyo ndivyo anaomba Mungu amsaidie kuliongoza kundi lake liweze kuurithi uzima wa Milele.

Baba Askofu Dkt. Shoo akiwabariki watheolojia wanne Moshi Mjini tarehe 06.03.2022