Mpango Mkakati Shirikishi 2023/2027 Waandaliwa

Kikao cha ufunguzi wa mchakato wa kuaanda Mpango Mkakati wa miaka 5 (2023-2027) wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini kimefanyika Uhuru Lutheran Hotel & Conference Center Novemba Mosi, 2022. Kilihudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo katika Ofisi Kuu ya Dayosisi, wakuu wa vituo vya Dayosisi, wakuu wa Majimbo pamoja na Makatibu wa Majimbo.

Mhe. Msaidizi wa Askofu Mchungaji Deogratius Msanya alifanya uzinduzi rasmi wa uandaaji wa mpango huo unaoongozwa na wataalamu wabobezi katika masuala hayo Dkt. Mshana, Dkt. Kimaro na Dkt. Matei.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alisema kuweka mipango ni utaratibu wa Mungu kuwa wanadamu wawe na Mipango katika kutekeleza yale ambayo ametutuma kuyafanya. Anasema neno la Mungu kutoka kitabu cha Mithali 29:18 Pasipo maono watu huacha kujizuia. Alifafanua kuwa kama hatuna Mipango tunakosa kujizuia na vilevile tunakosa nidhamu ya kuyaendea yale ambayo tunapaswa kuyatenda.

Alisema kuwa na mipango kunasaidia kuwa na nidhamu ya muda, rasilimali na fedha kwa sababu kunakitu ambacho tayari unakiona na unapaswa kukikamilisha.

Alitoa wito kwa wajumbe kushiriki kikamilifu katika kuandaa Mpango mkakakati ili waweze kuutekeleza kwa ufanisi na uaminifu.

“Naomba sana baada ya kumaliza kutengeneza Mpango Mkakati huu, yale yanayohusu  idara yako au mahali ambapo unasimamia uweze kueleza nini ambacho umekusudia kukifanya na niombe sana ushiriki wenu uwe kwa asilimia mia moja ili tuweze kupata mpango ambao ni makini, unaotekelezeka na ambao utatutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine”. Alisema Mch. Msanya

Akiwakaribisha wataalamu hao Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebadiah Moshi amesema mpango unaoandaliwa wa miaka 5 utatoa dira kufahamu jinsi tutakavyoweza kuisukuma Dayosisi ya Kaskazini kwenda pale tunapotaka ifike.

Alisema dhumuni la kukutana kwa pamoja ni kukubaliana na kuwa na uwelewa wa pamoja kufahamu ni wapi tunataka kuifikisha Dayosisi yetu kwa kipindi cha miaka.

“Tukishakubaliana kila mmoja kwa nafasi yake; mimi daktari, mimi nesi, meneja wa Uhuru Hoteli, Principal wa Chuo cha Biblia Mwika, tufanye nini kila mmoja kwa nafasi yake kuifanya Dayosisi yetu ifike pale tunapotaka kufika’’. Alihitimisha Mhandisi Zebadiah Moshi.

Baada ya ukaribisho, wataalamu hao walianza zoezi hilo la kuelimisha mambo 3 ikiwa ni Organization Capacity Assessment (OCA), Leadership Capacity Assessment (LCA) na Strategic Plan (SP). Zoezi la ukusanyaji wa maoni linaendelea kwa vituo vyote na majimbo yote.

Ufunguzi wa Uandaaji wa Mpango Mkakati wa Dayosisi wa miaka 5 (2023-2027)- Uhuru Hotel tarehe 01.11.2022