Mwinjilisti Kimaro Astaafu kwa Heshima, Atumika miaka 43

Mwinjilisti Julius Aleonasa Kimaro amestaafu kwa heshima baada ya kutumika katika huduma ya Uingilisti kwa miaka 43. Ibada ya kumstaafisha na kumuaga iliongozwa na Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Beniel Mallya katika Usharika wa Ng’uni (Oktoba 10, 2021).

Akizungumza mara baada ya kustaafishwa mwinjilisti Kimaro alisema, akitafakari safari yake ya utumishi katika huduma ya uinjilisti ameona jinsi Mungu alivyomtendea mambo mengi na kumtia nguvu kuweza kuifanya kazi yake kwa uamnifu hadi kustaafu kwa heshima.

“Mungu amenitia nguvu na kusimama nami wakati wote hata nilipojikwaa na kukutana na changamoto sikuwa pekee yangu Mungu alinipigania wakati wote” alisema Mwinjilisti Kimaro.

Anasema Mungu amemsaidia na kumwezesha kushinda katika hatari na maguma japo wakati mwingine alikata tamaa lakini roho wa Mungu alimkumbusha maneno haya ananukuu”Usiogope Tazama mimi nipo pamoja nawe hata utimilifu wa Dahari”alinukuu maneno kutoka Mathayo 28:20.

Aliwatia moyo watumishi waliopo shambani mwa Bwana kumtegeme Mungu katika huduma walioitiwa akiwaasa kudumu katika Maombi na kuwa watu wa kumsikiliza Roho Mtakatifu .

Mwinjilisti Kimaro alianza utumishi wake mwaka 1978 na kutumika katika sharika za Mroma, Nkwansira, Ngaya na Usharika wa Makorora na Kange huko Tanga. Sharika nyingine ni pamoja na Usharika wa Lemira Kati, Mafeto na Usharika wa Ng’u ni aliostaafu kwa heshima.