Parish Worker Isaria Lema Astaafu kwa Heshima

  • Parish Worker Isaria Lema Astaafu kwa Heshima
  • Atumika miaka 37
  • Askofu Shoo ampongeza kwa Utumishi mwema
  • Watoto washerekea Mikaeli na wa Watoto pamoja na Parish worker Isaria Lema
  • Watoto wawataka wazazi na walezi kuacha Ulevi
  • Mch. Mallyo: “Tutumie wakati tuliopewa na Mungu kwa uaminifu katika kazi na kuwa nuru ya ulimwengu”
  • Mohamedi Mkalipa alipongeza Kanisa kwa malezi ya watoto

Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Parish worker Isaria Noel Lema wa Usharika wa Nronga Jimbo la Hai la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Oktoba 8, 2023. Ibada hiyo iliambatana na maadhimisho ya sikukuu ya Mikaeli na watoto.

Parish worker Isaria Lema ametumika katika shamba la Bwana kwa takribani miaka 37 hadi anastaafu. Historia yake inaeleza kuwa Isaria Noel Lema alisoma Uinjilisti katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika mwaka 1981-1982.  Mwaka 1983 alihudumu katika Usharika wa Kawaya kama Mwinjilisti na Parish worker kabla ya kwenda kwenye masomo rasmi ya Parish worker katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika mwaka 1984-1985.

Baada ya kuhitimu masomo hayo mwaka 1986 alihudumu kama Parish worker katika Usharika wa Nronga pamoja na kufundisha Elimu ya Dini katika shule za msingi na masomo ya ufundi cherehani, shule ya Jumapili n.k hadi alipostaafu kwa heshima Oktoba 8, 2023.

Awali Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alimpongeza kwa utumishi wake ambapo alieleza kuwa amefanya kazi kubwa ya kuwafundisha watoto kufahamu msingi wa neno la Mungu utakaowasaidia kuwa nuru katika familia, jamii, Kanisa na Taifa.

Alisema watoto wanapopewa mafundisho yatakayowasaidia kuwaongoza kukua katika njia inayopasa kwa kuzingatia msingi wa neno la Mungu wanakuwa baraka katika familia na jamii kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Mallyo akihubiri katika ibada hiyo alisema tunapaswa kutumia wakati tuliopewa na Mungu ipasavyo katika kuifanya kazi yake kutimiza kusudi lake aliloweka kwa kila mwanadamu.

Alisema wanadamu wanapaswa kutambua kuwa Mungu ana kusudi au lengo la kumleta hapa duniani hivyo kuna haja ya kufahamu kusudi hilo na kulitimiza.

Alisema wazazi na walezi wana wajibu wa kuwasaidia watoto wao kufahamu kusudi/lengo la wao kuwepo hapa duniani ili waweze kulitimiza.

“Ni muhimu kuwaandaa watoto mara wanapokuja hapa duniani kutambua kusudi/lengo la wao kuwepo duniani, maana wanapotambua wataweza kutenda yaliyo mema na kuiweka jamii na taifa katika mstari mwema”. Alisema Mch. Mallyo.

Alihitimisha kwa kuhimiza kufanya kazi kwa bidii ikiwa bado mapema na tukiwa na nguvu kama neno la Mungu linavyotuasa kufanya kazi kwa bidii angali bado mchana akinukuu neno linavyotufundisha kuwa…  ‘Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja aspoweza mtu kufanyakazi” (Yohana 9:4).

Akitoa salam za pongezi kwa Parishwoker Lema; Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Amir Mohamed Mkalipa alimpongeza Mkuu wa Kanisa kwa jinsi anavyoweka mkazo mkubwa katika malezi ya watoto.

“Nimeshuhudia hapa jinsi watoto walivyoonyesha ukomavu katika mafundisho ya neno la Mungu na maadili kwa ujumla kupitia mashairi, ngojera na maigizo. Wamechukua sehemu kubwa ya hotuba yangu, wametuasa masuala ya ulevi na malezi kwa wazazi. Nampongeza mama yetu Lema kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa watoto hawa”. Alisema Mhe. Mkalipa.

Katika ibada hiyo watoto wa shule ya Jumapili walisheherekea sikukuu yao ya Mikaeli na watoto ambayo ilipaswa kufanyika Jumapili iliyopita lakini kwa heshima ya kumuaga mwalimu wao walisheherekea pamoja naye katika siku yake ya kustaafu.

Katika ujumbe wao kwa wazazi waliwaomba kuwajali, kuwalinda, kuwapa Elimu bora, kuwa na muda wa kukaa na familia na kuacha ulevi.

Kwa upande wake Parish Worker Lema aliwashukuru wote walioshirikiana naye katika utumishi wake. Pia aliwaomba wale wanaobaki katika kazi kuendelea kushirikiana, kupendana na kufanya kazi kwa umoja ili kazi ya Mungu isonge mbele.