Safari ya Miaka 40

Septemba 14, 2021 Mwinjilisti Donald Lema alihitimisha miaka 40 ya utumishi katika huduma ya Uinjilisti baada ya kustaafishwa rasmi kwa heshima na tendo hilo liliongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo katika Usharika wa Nronga Jimbo la Hai.

Safari ya huduma ya Uinjilisti ya miaka 40 ya Donald Lema ilianza Oktoba 4, mwaka 1981 alipobarikiwa kuwa Mwinjilisti mara baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika(1979-1980. Kama wasemavyo lenye mwanzo halikosi kuwa na Mwisho huduma yake alaiyoifanya kwa uaminifu aliihitimisha Novemba 14, 2021 alipostafishwa rasmi kwa heshima.

Mwinjilisti Lema anamshukuru Mungu kwa Neema ya pekee kumwita na kutumika katika huduma hiyo. Katika hotuba yake ya itikio anasema katika miaka 40 ya utumisha wake amekutana na changamoto nyingi lakini Mungu kwa Neema yake amemwezesha kufikia siku yake ya  kustaafu kwa heshima na kunukuu kitabu cha Zaburi ya 103:1  “Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyenzi Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake.

Alihitimisha kwa kulishuru Kanisa, watumishi wenzake  na washarika wote na kuwasii kuendelea kushirikiana na kupendana ili kazi ya Bwana inendelee kusonga Mbele.

Mkuu wa Kanisa alimshukuru Mwinjilisti Lema kwa utumishi wake uliotukuka katika shamba la Bwana. Alisema ni Mungu pekee ndiye aliyemjalia kufikia mwisho mwema  na kustaafu kwa heshima.

Kadhalika alitumia hadhira hiyo kukemea tabia ya baadhi ya watumishi wanaojiita ni manabii ambao wanafundisha mafundisho ya upotoshaji wa kweli ya neno la Mungu.”Leo kunamafundisho potofu yanayotolewa na manabii na walimu wa uwongo kwa tamaa zao wenyewe, wanahubiri mambo yanayofurahisha watu, mambo ya utajiri kwa maslahi yao binafsi”Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Amesema watu wenye kufanya mzaha na neno la Mungu ni dhihaka wanapasa kukemewa maana wanaweza kufanya hata taifa kuingia kwenye hasira ya Mungu.

Tusiache wala kuona haya kukemea, Neno la Mungu linawaonya kwamba Mungu hadhihakiwi maana hataacha kuadhibu dhambi na uasi.