Semina ya Watetezi Haki Yafanyika Umoja Lutheran Hostel

Semina ya watetezi haki za jinsia imefanyika Agosti 30, 2023 katika ukumbi wa mikutano Umoja Lutheran Hostel Moshi Mkoani Kilimanjaro ikihusisha maeneo mbalimbali ya vijiji  katika wilaya za Hai, Siha, Moshi Vijijini na Rombo.

Semina hiyo imewezeshwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini wakishirikiana na Dawati la Utetezi kutoka Makao Makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Mradi huo unatekelezwa pia katika Dayosisi ya Mbulu-Manyara, Dayosisi ya Kati-Singida na Dayosisi ya Kaskazini Kati-Arusha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Dawati la Utetezi KKKT Bibi. Besetina Saikong amesema lengo la semina hiyo ni  kutoka Elimu ya kuondoa ukatili  katika jamii ufahamu kuhusu migogoro.

Awali akifundisha mada kuhusu migogoro na utatuzi wa migogoro Bibi. Saikong alisema migogoro ni misuguano au kutokuelewana  baina ya pande mbili mfano mtu na mtu, kikundi na kikundi n.k.

Alisema migogoro inasababisha kukosekana kwa amani na hata kuzorotesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Alitaja mambo mbalimbali yanayoweza  kusababisha migogoro kuwa ni pamoja na  masuala ya kiuchumi, kisiasa,. umiliki wa raslimali, mahusiano na ukosefu wa Elimu au uelewa kuhusu jambo linaloweza kusababisha mgogoro.

Sababu nyingine alisema ni kukosekana kwa utawala bora na utawala wa sheria, mila na tamaduni zetu, ufinyo na uwiano usio sawa wa mgawanyo wa raslimali, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukabila, ubaguzi, kukosekana kwa maadili katika jamii, kukosekana kwa mahitaji muhimu kama maji, barabara, shule na kukosekana kwa taarifa muhimu na takwimu.

Kwa upande wake  Katibu wa Idara ya Wanawake na Watoto wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Faustine Kahwa akifundisha Mada ya pili kuhusu ukatili na Athari zake alisema watetezi hao wa haki wanapaswa kujituma kwa bidii katika kazi wanayoifanya ya utetezi kuweza kutokomeza ukatili katika jamii.

Alisema  wanapaswa kuwa mfano kuanzia nyumbani hadi katika maeneo yao ya kazi  katika kuondoa na kupinga ukatili kwa nguvu zote”Wewe kama Mama au Baba pale nyumbani kwako, anzia hapo kuondoa ukatili maana inawezekana ukawa mtetezi lakini pale nyumbani ukawa unafanya vitendo vya kikatili katika familia” Alisema Mch. Kahwa.

Mch. Kahwa aliwatia moyo watetezi hao katika kuifanya kazi hiyo na kuwataka kutokata tamaa hata pale wanapokutana na vikwazo.

“Niwaombe mkafanye Kazi, wasilianeni na wachungaji, mashehe kuzungumzia vitendo vya kikatili pale mnapovibaini na hata mkikwamishwa mahali nendeni ngazi inayofuata na tumieni mbinu mbalimbali”. Alisema Mch. Kahwa.

Katika mada yake alitaja baadhi ya aina za ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na Ukatili wa kimwili, Ukatili wa kisaikolojia, Ukatili wa kingono, Ukatili wa kiuchumi na Ukatili wa kiafya

Naye mmoja wa watetezi Haki Bibi. Amphorence Zakayo Mlay Kutoka kijiji cha Kahe alisema ukatili upo wa aina mbalimbali na anakutana na kesi nyingi za ukatili katika kijiji chak. Anasema kamati ya utetezi wamekuwa wakiendelea kutoka Elimu Katika maeneo mbalimbali kama misikitini, kanisani na hata siku za masoko kupunguza kasi ya vitendo vy kikatili.

“Juzi kimetokea kitendo cha kikatili sana hapa Kahe, mtoto wa miaka 2 aliokotwa umbali mrefu kutoka nyumbani anapoishi, umbali ambao mtoto huyo asingeweza kufika mwenyewe na aliokotwa akiwa ameshafariki pembezoni mwa mtaro na walipochunguza walibaini alilawitiwa na kesi hii tunaifatilia hivyo jamii watambue kweli vitendo vya kikatili ni vingi wasivifumbie macho” Alitoa ushuhuda Bibi. Mlay kuwa huo ni mfano wa vitendo vya kikatili wanavyokumbana navyo katika maeneo mbalimbali wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Katibu wa Idara ya Wanawake na Watoto KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. F. Kahwa (aliyesimama), akifundisha semina ya Watetezi Haki Agosti 30, 2023 Umoja Lutheran Hostel