Sikukuu ya Vijana na Uimbaji yafanyika Himo

Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya ameongoza Ibada ya Sikukuu ya Vijana na Uimbaji katika ngazi ya Dayosisi iliyofanyika katika Usharika wa Himo Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Oktoba 15, 2023 ambapo kwaya 24 zilishiriki sikukuu ya vijana na uimbaji.

Kwaya hizo ni kutoka katika Sharika na Vituo mbalimbali katika  majimbo 5 ya Dayosisi baada ya kufuzu kushiriki uimbaji katika ngazi ya sharika kanda na majimbo. Siku hii ya uimbaji katika ngazi ya Dayosisi hufanyika kila mwaka na huratibiwa na Halmashauri ya Liturugia na Uimbaji ya Dayosisi.

Akifungua mashindano hayo Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alisema waimbaji wanapaswa kutambua kuwa ili kumsifu Mungu kwa uzuri  inafaa kuimba wakiwa na Mioyo Minyofu. Alisema moyo mnyoofu ni mojawapo ya kanuni ya msingi ya kuzingatia katika kumsifu Mungu ukiacha kanuni ya kitaalamu.

Aidha alisema kuwa, kuimba kitaalamu ni kanuni nzuri ya kumsifu Mungu kwa uzuri lakini pasipo kuzingatia kanuni ya Unyofu wa Moyo kuimba au kusifu kwetu kunabadilika na kuwa kelele mbele za Mungu. Alihimiza kuwa tunapokosea kanuni ya unyoofu wa Moyo tunaathiri kanuni namba moja ya utaalamu katika kusifu

“Uzuri wa kumsifu Mungu ni kumsifu katika utakatifu, katika hali ya usafi. Tunapaswa kujitenga na uchafu na machukizo mbele za Mungu; waimbaji mnapaswa kumsifu Mungu katika usafi, angalieni Zaburi ya 33:1 wa kwanza inavyotukumbusha”.Alieleza Mch. Msanya.

Naye katibu wa Idara ya Vijana wanafunzi anayeratibu uimbaji Dayosisi Mch. Mathayo Mtui amesema Sikukuu ya Dayosisi imejejipanga kufanya matamasha na semina mbalimbali kwa vikundi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha  kwaya ili ziweze kutunga na kuimba nyimbo zenye kumsifu na kumtukuza Mungu.

Kwa upande wa waimbaji walioshiriki katika uimbaji akiwemo mwimbaji wa kwaya ya wanaume Usharika  wa Himo  Bw. Edward Shayo  alisema kuwa kipindi cha nyuma wanaume walikuwa hawana ari ya ushiriki tofauti na sasa ambapo amesema ari hiyo  inatokana na kuona faida ya kumwimbia Mungu.

Matokeo ya washiriki

Katika Uimbaji huo kundi la kwanza la Sekondari Mchanganyiko, nafasi ya kwanza ilishikwa na Shule ya Seminari Agape kwa alama 88 ikifuatiwa na mshiriki mwezake shule ya Sekondari Kilimatembo mwenye alama 80.

Kundi la pili lilikuwa la Sekondari Wavulana na nafasi ya kwanza ilishikwa na Shule ya Sekondari ya Wavulana Lyamungo kwa alama 76. Vilevile kundi la tatu la Vyuo Mchanganyiko Chuo Cha Biblia na Theologia mwika walishika nafasi ya kwanza kwa alama 83 ambapo pia hawakuwa na mpinzani.

Kwa kundi la nne la Kwaya za tarumbeta jumla ya kwaya zilizoshiriki zilikuwa 5. Nafasi ya kwanza ilishikwa na kwaya ya Usharika wa Sanya Juu na Uuwo kwa kufungana kwa alama 81, nafasi ya pili Usharika wa Hai kwa alama 82, nafasi ya tatu kwaya ya Karatu Mjini kwa alama 72 na nafasi ya tano ilishikwa na kwaya ya Usharika wa Moshi Mjini kwa alama 66.

Kundi la tano lilikuwa Kwaya ya Wanaume ambapo kwaya 5 zilishiriki. Nafasi ya kwanza iliongozwa na Usharika wa Himo kwa kupata alama 87 ikifuatiwa na kwaya ya Moshi Mjini kwa alama 86. Nafasi ya tatu kwaya ya Shiri kwa alama 82, nafasi ya nne kwaya ya Karansi kwa alama 80 na nafasi ya tano kwaya ya Karatu Mjini kwa alama 69.

Vilevile kundi la sita lilikuwa la Kwaya za Vijana Sharikani ambapo kwaya 5 zilishiriki. Katika kundi hili nafasi ya kwanza ilishikwa na Usharika wa Upperkitete kutoka Karatu kwa alama 85, ya pili Usharika wa Kingereka kwa alama 83. Nafasi ya 3 katika kundi hili ilishikwa na kwaya Himo kwa alama 76, ya nne Majengo alama 73 na nafasi ya tano Usharika wa Orkolili kwa alama 69.

Kundi la 7 lilikuwa Kwaya za Mchanganyiko Shariani, kundi hili pia lilikuwa na kwa tano. Nafasi ya kwanza kwa kundi hili iliongozwa na kwaya ya Usharika wa Kiboriloni kwa alama 89, ya pili Usharika wa Lyamungo Kati alama 85, ya tatu Usharika wa Lole kwa alama 83 na nafasi ya nne kwaya mbili za Usharika wa Sanya Juu na Rhotia zilifungana kwa alama 79.

Wataalamu walioshiriki katika kushauri pamoja na kutoa alama ni pamoja na Mch. Herzon Mashauri kutoka Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mwalimu Loi Kisiri kutoka Dayosisi ya Meru na Mwalimu David Mwera kutoka Anglikana Arusha.