Ni tamasha la pili la Funga Mwaka na Yesu tangu kuanzishwa kwa tamasha hili mwaka 2023. Lilifanyika siku ya Jumamosi tarehe 28 Disemba, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na kuhudhuriwa na Vijana wapato 9,458 wakike na wakiume.
Tamasha hili ambalo ni maalumu kwa vijana, huwapa fursa ya kutafakari maisha yao ya kiroho na kimaadili kwa mwaka mzima na kuhitimisha mwaka kwa neno, sala, maombi na nyimbo za injili.
Tamasha lilifunguliwa na Mkuu wa Dayosisi Ask. Dkt. Fredrick Shoo, maudhui ya mwaka 2024 yakitoka katika kitabu cha 1Petro 2:9 “Uzao Mteule” . Mnenaji alikuwa Mch. Nashon Kikalao.
Mbali na Neno la Mungu, vijana waliongozwa na waimbaji wa muziki wa Injili ikiwemo “Praise Team” ya Vijana wa KKKT Dayosisi Kaskazini, Rose Muhando na Boaz Danken katika kumsifu na kumwabudu Mungu.
Katika tamasha hili vijana walihimizwa kutunza utakatifu, kujibu maswali na changamoto zinazowakabili kama vile athari hasi za utandawazi, ukosefu wa ajira, kukata tamaa kunakopelekea vijana kujiua, matumizi ya pombe na madawa ya kulevya. Pia kijana kuvuka ujana bila makovu na hatimaye kurithi uzima wa milele.
Dayosisi inawashukuru wadau wote waliochangia kufanyika kwa tamasha hili, inawatakia vijana wote mwaka mwema wa 2025.