Tani 584 za Chakula zagawanywa kwa kaya zaidi ya 3700, Kisima cha Maji Chazinduliwa

Jamii zinazokabiliwa na ukame na njaa takribani kaya zaidi ya 3700 zimepokea misaada ya chakula, mbegu na wanyama kutoka Jimbo la Hai la KKKT Dayosisi ya Kaskazini wakishirikiana na shirika la Huyamwi la KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Zoezi hilo limezinduliwa rasmi na Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo Machi 10, 2022 katika Usharika wa Kia mtaa wa Yerusalemu.

Akisoma risala mbele ya Mkuu wa Kanisa Mkurugenzi wa Huyamwi Mdiakonia Samweli Mori amesema tani 575 za Mahindi na tani 9 za maharage zitagawanywa kwa nyakati tofauti  kwa washarika na wanajamii wa Kia, Nomeuti, Rundugai, Kawaya, Kikavu Chini na Magadini zinazokabiliwa na ukame na njaa.

Mbali na ugawaji wa mahindi na maharage amesema watagawa mbegu za mahindi na maharage kiasi cha tani 1100 na mbuzi 120 kwa wafugaji ambao mifugo yao imekufa kutokana na ukame. Kadhalika, watatoa semina 16 kuhusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Md. Mori amesema katika awamu ya kwanza Jimbo la Hai wakishirikiana na marafiki toka nje na Sharika za milimani waligawa gunia 64 za mahindi na 17 za maharage na Huyamwi kwa kushirikiana na marafiki waligawa zaidi ya gunia 100 za mahindi, gunia 23 za maharage na mikungu 80 ya ndizi katika Sharika hizo.

Baada ya uzinduzi wa zoezi la hilo, Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alizindua maji safi ya kunywa kutoka kisima kilichochimbwa na kuwekewa miundombinu kuwezesha upatikanaji wa maji. Kisima kimegharamiwa na Jimbo la Hai.

Baba Askofu Dkt. Shoo aliwashukuru wote waliojitoa kwa hali na mali kutoa misaada kwa Washarika na Wanaajamii wanaokabiliwa na ukame na njaa.

Amesema kumekuwa na ukame na uhaba mkubwa wa chakula katika maeneo mengi hasa maeneo ya tambarare “Tumeona na tumeshuhudia mifugo mingi ikifa na watu wengi wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na  sisi kama Kanisa katika utume wetu tumeona umuhimu wa kuwasaidia hawa wenzetu waliopatwa na njaa angalau kwa chakula ikiwa ni michango ya washarika na marafiki kutoka Ujerumani”Alisema Dkt. Shoo.

Alisema ukame nisehemu ya matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi. Amesema pasipo kuzingatia suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira majanga kama haya yatakuwa makubwa zaidi.

Baba Askofu Shoo alisistiza watu kuona umuhimu wa kuwa na akiba ya Chakula.

Njaa na uhaba mkubwa wa chakula katika sharika na jamii hii umekuja kutokana na ukame uliosababishwa na mvua kutonyesha mwaka 2021 na  kuendelea hadi sasa.

Baba Askofu Dkt. Shoo akionja maji mara baada ya kufungua kisima cha maji safi Usharika wa Kia mtaa wa Yerusalemu Machi 10, 2022