Tawi la USCF Chuo Cha Ushirika Moshi (MoCU) lazinduliwa rasmi.

Tawi la Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT-USCF la Chuo Cha Ushirika Moshi (MoCU) limezinduliwa rasmi katika Chuo cha Ushirika Moshi na Mchungaji mlezi wa USCF taifa Mch. David Kalinga Januari 30, 2022. USCF ni University Students Christian Fellowship.

 Akihubiri katika ibada hiyo Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya aliwataka wachungaji walezi kuwasaidia vijana waweze kumwona Yesu katika maishaa yao.

Mch Msanya katika mahubiri yake kutoka kitabu cha Yohana 12:21 ambalo ndilo lilikuwa neno Kuu, alifundisha akikaza maswali 5 yanayotoa majibu ya namna ya kumwona Yesu.

Swali la kwanza alisema unapaswa kujiuliza mimi ni nani ? Swali hili linalenga utambulisho wetu kuwa sisi ni wana wa Mungu na watumishi wa Mungu.

Swali la pili nimetoka wapi? Na kufafanua kuwa tumetoka kwa Mungu

Swali la tatu ninaweza kufanya nini? Na kufafanua kuwa ni nguvu yetu katika kutumika kwa ajili ya Mungu.

Swali la nne, kwanini nipo hapa? Alifafanua lengo la kuwepo ni kumtumikia Mungu na swali la tano ninaelekea wapi?  Jibu la swali ni hatima yetu  katika kurithi uzima wa milele. Mchungaji Msanya alisema  maswali hayo matano yanakusaidia kutenda yanayopaswa kuweza kumwona Yesu.

Kabla ya uzinduzi huo mwenyekiti wa USCF MoCU Bw. Samsoni Chacha Marwa alisoma risala ambapo alieleza kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa tawi hilo ulianza mwaka 2017.  ”Mchakato wa kuanzishwa tawi la USCF-MoCU ulianza mwaka 2017 na kuendelea hadi mwishoni mwa mwaka 2021, uongozi wa chuo Kikuu cha MoCU ulipokubali kuanzishwa kwa tawi hilo”.

Bw. Marwa alieleza kuwa tawi hilo limeanzishwa kwa lengo la kutangaza na kueneza injili, kuibua na kukuza vipawa na karama za vijana. Malengo mengine ni pamoja na kuwasaidia vijana kujikwamua na changamoto za kielimu, kimaisha kiuchumi , kupata vyombo vya muziki kuweza kutangaza injili katika maeneo mbalimbali hasa ya misioni.