TRA mkoa wa Kilimanjaro imeipongeza KKKT Dayosisi ya Kaskazini kupitia taasisi zake kwa ulipaji mzuri wa kodi kwa mwaka 2024.
Pongezi hizo ziliwasilishwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro Bw. James Jilala kwenye hafla ya mwisho wa mwaka ya Watumishi wa Dayosisi ya Kaskazini iliyofanyika Uhuru Lutheran Hotel and Conference Center Disemba 20, 2024.
Aidha Bw. Jilala alisema kuna umuhimu mkubwa wa kulipa kodi ili nchi iweze kujitegemea na kutoa huduma bora kwa jamii.
“Nitoe shukrani za dhati kwa Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwa ulipaji mzuri wa kodi kupitia hizi taasisi ambazo anazisimamia, ikiwemo Uhuru Lutheran Hotel and Conference Center na shule za Dayosisi kwa ulipaji mzuri wa kodi. Ombi letu ni kuendelea kuwa walipa kodi wazuri maana, wakati mwingine ukiambiwa wewe ni mlipa kodi mzuri, ukazoe ukashuka itakuwa sio vizuri kwa taifa.” Alisema Bw. Jilala.
Akipokea salamu hizo kwa niaba ya Askofu Dkt. Shoo, Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alisema Dayosisi inashukuru kwa kupata ujumbe ambao umekuwa ni faraja kwa Kanisa. Alisema kupewa mrejesho kwamba unafanya vyema ni jambo jema.
Aliwapongeza TRA kwa kuleta mrejesho huo kwamba Kanisa linafanya vizuri katika wajibu muhimu wa kulipa kodi kama raia wema.
“Tunafahamu katika zile amri kumi tulizopewa, amri ya saba inasema usiibe, usipolipa kodi ni kuiba na mara nyingine tunataka huduma bora lakini kodi hatulipi. Serikali haiwezi kutoa huduma bora kwa raia wake kama raia hawalipi kodi, kwa hiyo tunashukuru kwa mrejesho huu, umekuwa faraja kubwa kwetu na nitafikisha ujumbe huu kwa mkuu wa Dayosisi kwamba tumepata watu ambao wamefika wakatutia moyo kwamba tunafanya vizuri.” Alisema Mch. Msanya.
Aidha Mch. Msanya alipongeza TRA kwani kwa sasa zoezi la ukusanyaji kodi limekuwa rafiki tofauti na awali na aliomba zoezi hili liendelee kuwa rafiki.

