Tusiache Kumshukuru Mungu

Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo amesema kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo, kwa sababu Mungu ni Mungu na hakuna mbadala wake na ndiye pekee anayestahili kushukuriwa.

Alisema hayo kwenye Kongamano la kumshukuru Mungu kwa Maisha na Utumishi wa Hayati Rais Dkt. John Magufuli na kuliombea Taifa lililofanyika Aprili 18, 2021 mjini Dodoma akitoa mada kuhusu sababu za kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo lililoandaliwa na viongozi wa Dini Nchini, alikuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi.

Askofu Dkt. Shoo alisema, katika Biblia takatifu kitabu cha Wathethalonike wa kwanza kinasema Furahini siku zote, ombeni bila kukoma , Shukuruni kwa kila jambo maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu,

“Kwa kuwa Mungu ni Mungu na nimuweza wa yote na maamuzi yake hayahojiwi na ndiye anayebeba uhai wetu, maisha yetu, uwezo wetu na vyote viko mikononi mwake na tunaamini anatupenda na hafanyi lolote kanakwamba anatuchukia, tunapaswa Kumshukuru kwa kila jambo.”Alisema Dkt. Shoo.

Hivyo alisema tunapaswa kumshukuru Mungu kwa Maisha ya hayati Rais John Joseph Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021.

Kwa niaba ya viongozi wa dini alisema kuwa watamwombea na kumpa ushirikiano rais Samia Suluhu Hassan na rais Dkt Hussein Mwinyi, kuhakikisha taifa linakuwa na ustawi kiroho, kimwili na kiakili kama taifa moja.

Watatu kulia ni Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwenye kongamano la viongozi wa Dini mjini Dodoma