Tusifanye Kazi kwa Unafiki: Askofu Dkt. Shoo

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amewataka watumishi wa Ofisi Kuu na Dayosisi kufanya kazi kwa uaminifu bila unafiki katika kutimiza majukumu yao. Askofu Shoo aliyasema hayo akiongea na watumishi wa Ofisi Kuu ya Dayosisi katika ibada ya kufungua Ofisi katika chepo ya ofisi kuu Januari 4, 2023.

Askofu Dkt. Shoo amesema hatupaswi kufanya kazi kwa unafiki au kufanya kazi kwa bidii kwa sababu fulani au mkuu wako anakuona bali tufanye kwa uaminifu tukijua tunamtumikia Mungu.

Tutambue tunamtumikia Bwana Yesu Kristo na si wanadamu hivyo, tunapaswa kutumika kwa uaminifu na uadilifu akinukuu neno kutoka kitabu cha Wakolosai 3:23 ‘Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na siyo wanadamu’.

“Tusidhulumu katika kutega, tuzingatie muda, tusibie kwa muda au kwa namna yeyote kwa maana neno la Mungu linatuambia  adhulumuye atapata ujira wake” Alisema Askofu Dkt. Shoo

Alisema tuzidi kumwomba Mungu atusaidie tutumike kwa uaminifu na kwa moyo tukijua tunamtumikia Mungu. “Ukimtumikia kwa uaminifu, ujira wako utabarikiwa, Mungu atusaidie kufanya kwa uaminifu tukiombeana sisi kwa sisi ili Mungu atufanikishe na mahali hapa pawe pa baraka” Alihitimisha Askofu Dkt. Shoo.