TUWEKEZE KWA WATOTO NA VIJANA KWA KUWAFUNDISHA MAADILI MEMA

Mkuu wa KKKT  Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Frederick Onael Shoo, amesema ni vyema  Kanisa likahakikisha  kuwa waalimu wanaowafundisha watoto vipindi vya dini Makanisani waandaliwe vizuri ili wawafundishe misingi imara itakayowasaidia katika maisha yao ya sasa  na ya baadaye.

Askofu Shoo aliyasema hayo kwenye ibada ya uzinduzi wa usharika mpya wa Pumuwani, jengo la ibada kwa watoto na nyumba ya Mchungaji iliyofanyika katika Usharika  huo Julai 7, 2024.

Alisema ili kuwa na jamii imara na taifa imara ni lazima watoto na vijana wawe wamepata mafundisho yenye maadili.

Awali  akihubiri  katika  ibada hiyo Msaidizi wa Askofu KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Deogratius Msanya, aliwataka wazazi, walezi  na kanisa kuhakikisha kuwa wanawaandaa vijana ili waweze kujitambua na wawe na mchango katika jamii inayowazunguka na kanisa kwa ujumla .

Alisema vijana wengi amejiingiza katika michezo ya kubeti badala ya kufanya kazi. “Niwaonye vijana, achenio michezo ya kubeti, mafanikio ni kuweka mipango na kufanya kazi kwa bii na kamwe hayaji kwa beti… Wazazi tuwafundishe Vijana Stadi za Maisha  waweze kufanya kazi kwa bidii na kuacha kubeti, mzingatie kuwa mafanikio hayaji kwa kubeti yanakuja kwa mipango na juhudi katika kazi”Alisema Mch. Msanya.

Kwa mujibu wa msoma risala ya uzinduzi  wa usharika huo Bibi. Neema Ulungi alisemaema kuwa usharika huo ulianza mwaka 1963 ukiwa kama mtaa ambapo wakristo walikuwa wakisali katika kanisa Dogo na mwaka 2023 ukapata kibali cha kuwa Usharika.