Usharika Mpya Bethel Msufini wazinduliwa

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael shoo, amezindua rasmi Usharika mpya wa Bethel Msufini Jumapili ya Novemba 13, 2022. Kabla ya kuzinduliwa kwa Usharika huo Baba Askofu Dkt. Shoo aliweka wakfu kwa-kupiga rato eneo ambalo Kanisa la Mtaa wa Ebenezer wa Usharika wa Bethel Msufini litajengwa. Usharika wa Bethel Msufini umegawanyika kutoka Usharika wa Msaranga Mandaka.

Kuanzishwa kwa Usharika wa Bethel Msufini:

Mkutano Mkuu wa 4 wa Usharika wa Msaranga Mandaka uliofanyika mwaka 2020 uliazimia kuanzisha Usharika mpya wa Bethel Msufini. 

Chini ya uongozi wa marehemu Mchungaji Dalem Lyatuu mnamo mwaka 2010 eneo la usharika huu mpya wa Bethel Msufini lilipatikana. Wakati huo Bethel ikianzishwa kama mtaa wa Msaranga Mandaka. Baada ya kupatikana kwa eneo, msingi ulijengwa na jiwe la pembe liliwekwa rasmi Disemba 31, 2011 na Mkuu wa Dayosisi wakati huo Askofu Dkt. Martin Fuatael Shao.

Jitihada ziliendelea za kiongozi aliyefuata Mch. Sheckland Foya za kuweka hema juu ya Msingi uliowekwa na shughuli rasmi za kiibada zilianza Machi 10, 2013. Ibada hiyo ya saa 4 ilihudhuriwa na washarika wapatao 134 na watoto 4.

Jitihada mbalimbali ziliendelea kufanywa na viongozi mbailimbali waliohudumu katika Usharika wa Msaranga Mandaka katika kuukuza, kuuimarisha na kuendeleza Mtaa wa Bethel kuwa Usharika uanaojitegemea. Na mnamo Januari Mosi, 2022 Betheli ilizaliwa rasmi kuwa Usharika wa Bethel Msufini ukiwa na washarika 744 kutoka 134 ulipokuwa mtaa mwaka 2013.

Akizindua Usharika huo Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, aliupongeza Usharika wa Bethel Msufini kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja tangu walipoazimia kuanzisha usharika huo.

“Napenda kumshukuru Mungu kwa kuwa ameifanya siku hii, kumekuwa na Ibada ya uzinduzi wa Uhsarika, kupiga rato eneo la mtaa wa Ebenezer, uzinduzi wa Biblia ya Kimochi na kumstaafisha mwinjilisti Joseph Ngowi, hii ni heshima kubwa. Ninawapongeza sana, mmeanza kuwa Usharika mwezi wa kwanza lakini tumeona   kazi kubwa”Alisema Dkt. Shoo

Alisema Umoja wao, upendo na ushirikiano ndivyo vitakaowawezesha kusonga mbele kama usharika. “Sina mashaka ninaamini usharika huu utazidi kusonga mbele na utakuwa usharika wa mfano wa kuigwa” . Alihitimisha pongezii zake.

Katika risala iliyosomwa na Mchungaji kiongozi wa usharika huo, alisema hadi kukamilika kwa jengo hilo la Kanisa litagharimi kiasi cha shilingi bilioni moja.

Wamochi wazindua Biblia

Katika Ibada hiyo pia Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alizindua Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya kimochi, tafsiri iliyofanywa na wataalamu kutoka Chama cha Biblia Tanzania.

Awali kabla ya uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Tanzania Dkt. Alfred Kimonge alisema kwa hapa Tanzania wamekamilisha tafsiri za lugha 10 za Biblia, lugha 40 agano jipya, lugha 18 sehemu ya Biblia kati ya lugha 132. Anasema Mpango ni kuafikia lugha zote.  Aidha alitoa rai kwa wanajamii wa lugha husika kutumia Biblia za kilugha mara nyingi kadiri iwezekanavyo ili kazi ya utafsiri isiwe ni kazi bure.

Askofu Dkt. Shoo aliwashukuru kwa kujitoa na uvumilivu wa kazi hiyo ya kutafsiri katika lugha  mbalimbali. Amewaomba kufikiria kutafsiri Biblia nyingine kwa lugha ya Kisiha. Alihimiza kuwa tafsi hizo za lugha mama ni njia ya kudumisha na kuhuisha lugha zetu ambazo Mungu ametupa.

125 Wahitimu ETE

Katika Ibada hiyo jumla ya wahitimu 125 walihitimisha mafunzo yao ya Elimu ya Theologia Enezi kutoka katika sharika mbalimbali za majimbo ya Dayosisi. Elimu ya Ete kwa mujibu wa risala ya wahitimu ipo katika misingi ya kumfuata Kristo, kuwaleta watu kwa Yesu na kufundisha Imani na kweli ya neno la Mungu na mafundisho ya kweli ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri.

Mwinjilisti Ngowi astaafu kwa Heshima

Pia katika Ibada hiyo Mwinjilisti Joseph Ngowi alistaafishwa kwa heshima baada ya kutumika kwa miaka 33 katika sharika mbalimbali za Jimbo la K/Kati hadi kustaafu akihudumu kwake akiwa anahudumu katika Usharika mpya wa Bethel Msufini. Alisoma Uinjilisti katika chuo cha Biblia na Theologia mwika mwwaka 1989 hadi 1992.

Katika Ibada ya ufunguzi wa Usharika wa Bethel Msufini