Usharika Mpya KKKT DK Wazinduliwa Rasmi

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amezindua rasmi Usharika mpya wa Ghona uliopo Jimbo la Kilimanjaro Kati la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Januari 22, 2022.

Kabla ya uzinduzi huo, Baba Askofu aliweka jiwe la pembe jengo la Kanisa mtaa wa Darajani ndipo alipoelekea Senta ya Usharika wa Ghona kuzindua Usharika, kuweka jiwe la pembe na kuweka wakfu kanisa.

Katika matendo hayo, Baba Askofu alishirikiana na Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mch. Javason Mrema na Mch. Kiongozi wa Usharika huo Mch. Emmanuel Swai.

Kwa mujibu wa Mchungaji kiongozi wa ushaarika wa Ghona Emmanuel Swai, alisema usharika huo ulianzisha rasmi huduma za ibada Januari mosi 2022 na una jumla ya mitaa 6 na washarika 1351 hadi sasa (watu wazima 851 na watoto 500).

Katika Ibada hiyo, Baba Askofu Dkt. Shoo alitumia hadhira hiyo kuwataka Wakristo kuwa mfano wa kuigwa na mstari wa mbele katika kupinga na kukataa ubaguzi kama Yesu alivyofundisha kwa vitendo.

Alisema kukataa na kupinga ubaguzi pekee haitoshi, tunapaswa kwenda mbali zaidi kwa kukataa kushiriki aina yeyote ile ya ubaguzi. Anasema Yesu Kristo amekuwa mfano kwetu sisi wa kupinga ubaguzi akitoa mfano wa Yesu alipokutana na Mwanamke Msamaria katika Kisima akimwomba maji anywe kinyume na ilivyokuwa kwamba Wayahudi hawachangamani na makabila mengine.

Alisema Biblia inatuonyesha jinsi wayahudi walivyowabagua na kuwatenga makabila mengine wakiona kwamba ahadi na baraka za Ibrahimu ni za Wayahudi pekee.

“Waliwatenga mfano majirani zao Wasamaria kwamba hawakustahili kushiriki Neema za Mungu, na endapo ukitaka kushiriki nao ulipaswa kuitimiza torati, tamaduni zao mfano kutahiriwa kama wayahudi n.k ndipo uweze kushiriki.

Alisema Mtume paulo anasema katika kitabu cha Wagalatia 3: 23-29 kuwa, Yesu alikuja kayaondoa yote kwamba hatuhesabiwi haki kwa kufuata na kuishika torati bali ni kwa njia ya imani pekee.

“Hatuhesabiwi haki kwa torati, ni kwa Imani maana kwa njia ya Imani tumemvaa Kristo; Kwa njia ya imani, makabila yote bila kujali wewe ni myahudi, muyunani n.k, sote tunakuwa uzao wa Ibrahamu na tunashiriki ahadi na baraka za Ibrahimu alizopewa na Mungu”. Alisema Dkt. Shoo.

Awali aliwapongeza Washarika wa Ghona, Uongozi na Baraza la Usharika kwa kazi nzuri waliyofanya “Tumeshuhudia kazi kubwa na nzuri ambayo mmefanya washarika wa Ghona, nawapongeza sana kwa matendo ya kuweka jiwe la pembe mtaa wa Darajani, uzinduzi wa Usharika na kuweka wakfu nyumba ya Ibada; Tunaweza kusema ghona leo mmepata kipaimara hongereni sana” Alisema Dkt. Shoo.

Aidha aliwaomba waendelee kuifanya kazi ya Bwana kwa umoja na kuendelea kustawi kirohoo ili Mungu aendelee kutenda kazi yake na miujiza yake.

Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo akiweka jiwe la pembe jengo la Kanisa Mtaa wa Darajani Usharika wa Ghona, Januari 22,2023