Usharika Mpya wa Kanaani Lombeta wazinduliwa rasmi,

Usharika Mpya wa Kanaani Lombeta wazinduliwa rasmi, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini ASkofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amefungua rasmi Usharika Mpya wa Kanaani Lombeta pamoja na kuweka jiwe la msingi jengo la ibada kwa watoto wa shule ya Jumapili Machi 12, 2023. Baba Askofu shoo aliongoza ibada hiyo akishirikiana na Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa Jimbo la K/Kati Mch. Javason Mrema na Mch. Kiongozi wa Usharika huo Mch. Arnord Temu. Pia katika ibada hiyo kulikuwa na huduma ya ubatizo wa mtoto mmojaAwali Baba Askofu Shoo aliwapongeza washarika wa Kanaani Lombeta kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya usharikani hapo na kwa namna wanavyojihusisha katika suala la utunzaji wa Mazingira kama neno la siku linavyohimiza kutunza Mazingira (Kumbukumbu la Torati 20:19). Dkt. Shoo alisema Mungu aliumba mbingu na nchi, na kuweka vyote vilivyopo na kisha kumweka mwanadamu katika bustani ya edeni kuilima na kuitunza akimaanisha wajibu wa kwanza aliopewa mwanadamau na Mungu ni kuwa wakili wa kutunza uumbaji wake.Alisema katika kitabu cha zaburi ya 20 na 28 kinasema hii dunia ni mali ya Mungu na wala sii mali yetu. “Dunia imeumbwa kwa ustadi mkubwa na kuweka uhai kwa wanyama na mimea na vyote vikitegemeana, hivyo mwanadamu anapoangamiza viumbe vingine mwisho wake naye hatoweze kuishi katika dunia hii” Alisema Dkt. Shoo.Alisema kwa sasa dunia imeanza kuona matokeo ya uharibifu wa mazingira “Kwa uzoefu wangu sijapata kuona kiasi kikubwa cha joto hapa Kilimanjaro kama ilivyo sasa, majira ya mvua na kiangazi yamebadilika, na haya ni matokeo ya uharibifu wa mazingira” Alisema Askofu Dkt. Shoo.Alitoa Wito kwa jamii kukumbushana na kuchukua hatua ya kuotesha miti yakutosha na kulinda vyanzo vya maji.Pia aliwakumbusha Wachungaji katika sharika zote za Dayosisi kusimamia kikamilifu sera yetu ya kila mtoto anapoanza kipaimara aoteshe na kutunza miti 10 kabla ya kubarikiwa. Kuanzishwa kwa Usharika wa Kanaani LombetaMkutano Mkuu wa 4 wa Usharika wa Msaranga Mandaka uliazimia kwamba usharika huo ugawanyike na kuwa sharika 3 ambazo ni Usharika wa Msaranga Mandaka, Betheli Msufini na Kanaani Lombeta na kukubaliwa na vikao rasmi vya Jimbo na Dayosisi ndipo ilipofika Januari Mosi, 2022 sharika hizi zikaanza rasmi. Kwa mujibu wa Mch. Kiongozi wa Usharika wa Kanaani Mch. Arnord Temu, Usharika huu una jumla ya mitaa 2 na umeanza ukiwa na washarika 794 (watu wazima 557 na watoto237).

Baba Askofu Dkt. Shoo akimbatiza Mtoto siku ya ufunguzi rasmi wa Usharika wa Kanaani Lombeta, Machi 10. 2023