Usharika wa Longuo wafunguliwa, Katibu wa Jimbo aingizwa Kazini, Mwinjilisti Astaafishwa kwa Heshima

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amezindua Usharika wa Longuo Jimbo la Kilimanjaro Kati katika ibada ya Jumapili ya Agosti 22, 2021 baada ya ujenzi na ukarabati uliofanywa na kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 200 kukamilika.

Tendo hilo lilifanyika sanjari na uzinduzi wa nyumba ya mchungaji iliyogharimu Shilingi za Kitanzania milioni 15.5 pamoja na jiko na ofisi ya vijana vilivyogharimu milioni 30.6 za Kitanzania.

Ujenzi wa Kanisa na Nyumba ya Mchungaji uligharamiwa na michango ya  washarika wote wa Longuo walio nje na ndani pamoja na marafiki huku jiko na ofisi ya vijana vimejengwa kwa kugharamiwa na Idara ya Wanawake na Vijana usharikani hapo.

Katibu  wa Jimbo Aingizwa Kazini, Mwinjilisti Astaafishwa

Katika hatua nyingine Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alimwingiza Kazini Katibu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Bw. Regnald Hosea baada ya kuitwa kushika nafasi hiyo iliyokuwa wazi kutokana na aliyekuwa Katibu wa jimbo hilo Mwinjilisti Aisario Mrema kustaafu.  

Baada ya tendo la kumwingiza Kazini Katibu wa jimbo, Mwinjilisti Gladson Maeda alistaafishwa kwa heshima baada ya kutumika kwa miaka 36 kama mwinjilisti katika sharika mbalimbali za Jimbo na Misioni ya huko Morogoro ambapo tendo hilo pia lilifanywa na Baba Askofu Dkt. Shoo.

Akihubiri katika ibada hiyo iliyoongozwa na kichwa cha somo  matumizi ya ulimi, Baba Askofu Shoo aliwataka Wakristo na jamii kutumia vizuri ndimi zao kwani maneno  yana nguvu kubwa ya kuharibu sifa na kubomoa mahusiano baina ya watu.

Amesema matumizi mazuri ya ulimi ni jambo la muhimu katika ustawi wa maisha yetu pale unapotumika vizuri “Ulimi unamtukuza Mungu, unamhimidi Mungu na kuwa baraka lakini kwa ulimi huo huo tunawalaani wenzetu na kuleta maumivu  vilevile kuharibu mahusiano ya watu.

Ameonya kuacha kutumia ndimi zetu kuleta maneno yanayoumiza na kuleta mafarakano badala yake tuzitumie kuleta utukufu wa Mungu. Kawasihi Wakristo kumwomba Mungu awasaidie waweze kutumia ndimi zao na kuzitawala ili waweze kuwa baraka.

Aidha amewaasa waamini kuwa waangalifu na kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie na kuwajalia Neema ya kuweza kuwatambua wanaojiita ni manabii wanaotumia ndimi zao kuwapotosha watu katika kweli ya Neno la Mungu. “Wapo watu kila akikwambia kitu anakwambia ameongea na Mungu kwenye ndoto; muwe makini wengine ni ndoto zao tu, Mwombeni sana Roho Mtakatifu awape uwezo wa kupambanua ni lipi neon la kweli na sauti ya kweliu inayotoka kwa Mung”.Alisema Dkt. Shoo

Akihitimisha Mahubiri yake alimpongeza Mchungaji kiongozi wa Usharika Mch. Richard Njau kwa kazi kubwa aliyofanya kwa kipindi kifupi cha kuwepo kwake pamoja na viongozi na washarika wote wa Longuo.

Pia alimpongeza Mwinjilisti Gladson Mamuya kwa kutumika kwa uaminifukwa kipindi chote hadi alipostaafu na kumtakia baraka. Pia alimtakia baraka njema Katibu wa Jimbo katika utumishi wake Mungu aliomwitia.

Msaidizi wa Askofu Mstaafu Mch. E. Saria (Kulia), Kaimu Katibu Mkuu Bw. Munguatosha Makyao (wapili kulia) Katika Ibada Longuo