Ni semina ya wiki mbili ya walimu takribani 56 wa Shule za Montensori zinazofundisha kwa njia ya vitendo iliyofanyika katika Chuo cha Walimu wa Montensori Ushirika wa Neema. Kati ya walimu hao 56 waalimu 28 wanatoka shule za msingi na awali za Halmashauri ya Wilaya ya Siha na wengine 28 wanatoka katika vituo vya Kanisa na binafsi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Semina hiyo ni mwendelezo wa warsha ya siku moja ya zaidi ya walimu wakuu 70 na maafisa Elimu 6 kutoka wilaya ya Siha waliokutana chuoni hapo mwezi Julai, 2023 kwa lengo la kujengeana uwezo wa ufundishaji kwa njia ya vitendo na utengenezaji wa zana za kufundishia katika shule za awali, msingi na vituo vya Montesori. Baada ya warsha hiyo ndipo walimu wakuu na maafisa elimu hao wakakubaliana kuwaleta waalimu kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa mfumo wa vitendo na kutengeneza zana za kufundishia.
Naye mgeni Rasmi Bibi Florence Ngowi Afisa Elimu takwimu na vifaa wilaya ya Siha akizungumza na wanasemina hao; awali alitoa Pongezi kwa Chuo hicho kwa jinsi wanavyoshirikiana na shule za serikali na vituo binafsi katika suala la kutoa elimu ya utengenezaji wa zana za Montesori na kutoa mafunzo ya ufundishaji kwa vitendo.
Bibi. Florance aliwasihi walimu hao mara baada ya semina waende kusia mbegu ya ujuzi na maarifa waliyoyapata kwa walimu wengine katika shule wanazotoka bila choyo.
“Mkayaambukize haya maarifa kwa wenzenu, najua mmetoka maeneo mbalimbali hivyo ni matarajio yangu ujuzi huu utasambaa katika mkoa wetu wa Kilimanjaro. Msiweke kabatini ujuzi mlioupata hapa, mkatumie ujuzi huu na zana, kwa uangalifu na kwa ufanisi katika kuwafundisha watoto”. Alihimiza Bibi. Florance.
Aidha alihimiza walimu hao kuhusu utunzaji wa zana walizotengeneza wakizingatia kujenga urafiki, mahusiano mazuri na upendo kwa watoto.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Mwalimu Lilian Kimaro alisema Semina hiyo imelenga kuwafudisha na kuwajengea uwezo waalimu wa madarasa ya montesori kujifunza kufundisha na kutengeneza zana za kufundisha kwa njia ya vitendo.
“Mafunzo haya ni muhimu kwa ajili ya kuwakumbusha walimu na kuwarejesha kwenye mstari kwa kukumbushana mbinu bora za kufundisha na kutengeneza zana bora. Walimu wakitumia zana za kufundishia ni njia rahisi ya kumsaidia mototo kuelewa na kukumbuka kwa urahisi ukilinganisha na njia hii ya kawaida isiyotumia zana.” Alieleza Mwalimu Lilian.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu mwalimu Ibrahim Magi alisema miongoni mwa mambo waliyojifunza ni pamoja na kujifunza mbinu bora za ufundishaji, kutengeneza zana za ufundishaji kwa njia ya vitendo, mbinu za kuibadilisha jamii kuwa jamii yenye mtazamo chanya katika kulea na kufundisha watoto. Pia kuwa mfano bora kwa jamii na mbinu za kujenga urafiki kwa watoto.