Vijana Tumieni Nguvu Zenu Kwa Uadilifu: Askofu Dkt. Shoo

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amewataka vijana kutumia nguvu zao kwa uadilifu katika kujenga maisha yao, ya Kanisa na Taifa kabla nguvu za ujana wao hazijaisha. Askofu Dkt. Shoo aliyasema hayo Disemba 15, 2022 akifunga Juma la Askofu na Vijana lililofanyika katika Sekondari ya Ufundi Moshi kuanzia Disemba 12, 2022.

Alisema Vijana wanaweza kulijenga Taifa na Kanisa la Mungu endapo watazitumia nguvu zao kwa faida  kwa kufanya mambo ya maana kama vile: Kusoma kwa bidii, kujenga vizuri, kuwasaidia wazazi, walezi na ndugu wenye mahitaji, kumtumikia Mungu kwa kutoa Sadaka, kuimba kwaya, kuhubiri, kutunza mazingira kwa kulinda vyanzo vya maji, kuotesha miti ya mbao, matunda, kuweka akiba kwa ajili ya siku zijazo, kufundisha wengine n.k. kabla nguvu za ujana wao hazijaisha.

 “Nguvu za kijana ni za mpito. Kijana hawezi kuamua kudumu katika ujana na kuendelea kuwa na nguvu alizo nazo siku zote za maisha yake. Ndio maana waswahili walisema “Ujana ni maji ya moto” Maji ya moto hupoa. Umri unavyosonga nguvu za ujana huanza kupungua, ni kutake kijana popote pale ulipo tumia nguvu zako vizuri kabla hazijaisha”. Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Askofu Dkt. Shoo alisema Taifa, Kanisa na jamii linawategemea vijana katika ustawi wake na ili hili litimie tunahitaji vijana wenye uzalendo wa dhati kwa familia, jamii, Taifa na Kanisa la Mungu.

“Inasemekana kuwa wazee wa kiafrika walizaa watoto wengi kama sehemu yao ya kuweka akiba ili watoto wawatunze wakati wa uzee, hii dhana inadhihirisha nguvu ya ujana katika kujenga familia, taifa na Kanisa la Mungu”

Dkt. Shoo anasema kijana asipojiandaa vizuri katika kufanya kazi kwa bidii na kuweka akiba wakati wa ujana, atakuwa amejiandaa kuwa na maisha magumu wakati wa utu uzima na wakati wa uzee.

Katika hitimisho lake, Baba Askofu Shoo alisema vijana wanapaswa kujitambua na kusimama katika nafasi zao ili nguvu zao zitumike kwa utukufu wa Mungu na  kunukuu maneno kutoka kitabu kitakatifu cha  Biblia akisema“ Mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu wakati wa ujana…” (Mwa.8:21 b)

“Kila kijana avunje rekodi kwa kuutafuta uso wa Mungu yaani Mapenzi ya Mungu kwa kufanya kazi kwa bidii, kutoa sadaka, kuweka akiba na kujiepushe na makundi mabaya”. Alihitimisha Askofu Dkt. Shoo.

Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebhadia Moshi akiwasalimu Vijana katika Juma la Askofu na Vijana Disemba 15, 2022