Vijana Wahimizwa Kuishi Maisha ya Kumcha Mungu

Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mch. Deogratius Msanya amewahimiza vijana kuishi maishi ya kumcha na kumtegemea Mungu wakati wote.

Mch Msanya aliwaasa vijana hao akihubiri kwenye ufunguzi wa Juma la Askofu na Vijana katika shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi Jumanne ya Disemba 13, 2022 mbapo takribani vijana 400 wamehuzuria kutoka katika sharika za Dayosisi.

Msanya amewakumbusha vijana kuwa Mungu kawaita kwa majina yao na kuwachora kwenye viganja vya mikono yake hivyo wanapaswa kutambua kuwa Mungu daima yupo pamoja nao na anawapenda.

“Kijana  wewe ni wapekee, ni mheshimiwa maana Mungu anakupenda  na kukulinda siku zote hata pale mnapopita katika majiribu anakuwa pamoja nawe” Alisema Mch. Msanya.

Anasema sisi kama waamini majaribu na changamoto ni sehemu ya maisha yetu. “Wakati mwingine tunahisi kuwa  Mungu yupo mbali nasi tunapopita katika majaribu na hata kuathiri imani yetu lakini tujue kuwa haya majaribu tunayokutana nayo sisi waamini na kutikisa imani zetu, Mungu bado  yupo pamoja nasi” Alikaza Mch. Msanya

Juma la Askofu na Vijana hufanyika kila mwaka ambapo vijana hupata fursa ya kujifunza neno la Mungu na mada mbalimbali. Mwaka huu limefanyika kuanzia Disemba 12 hadi 16.