WACHUNGAJI WAPATA PIKIPIKI KUWASAIDIA KATIKA HUDUMA

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo, amegawa pikipiki 7 kwa wachungaji toka sharika mbalimbali watakazozitumia katika kufanya huduma sharikani.

Baba Askofu Dkt. Shoo aligawa pikipiki hizo ikiwa ni utaratibu ambao Dayosisi imekuwa ikifanya kuwawezesha wachungaji kupata pikipiki kwa njia ya uenyeji na kwa bei nafuu.

Pikipiki moja inagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni mbili na laki tatu (2,300,000/=) ikiwa imekatiwa vibali vyote ambapo mchungaji anapewa kwa unafuu wa nusu bei sawa na shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000/=) badala ya milioni mbili na laki tatu.

Zoezi hilo lilifanyika katika ofisi kuu ya Dayosisi ya Kaskazini Julai 20, 2021 ambapo mchakato wake huratibiwa na ofisi ya Msaidizi wa Askofu ikishirikiana na ofisi ya Boharia.

Mchakato wa upatikanaji wa pikipiki hufanyika kwa Wachungaji wanaohitaji kuandika barua ya maombi kwa ofisi ya Msaidizi wa Askofu kisha kujadiliwa katika vikao na wanaokidhi hupewa pikipiki.

Aidha kabla ya kupewa pikipiki mwombaji atapaswa kulipa asilimia 10 ya gharama ndipo akabidhiwe pikipiki na sehemu inayobaki ya deni italipwa kwa kipindi kisichozidi miezi ishirini na nne. Mara baada ya kumaliza deni lililobaki pikipiki inakuwa mali binafsi ya mchungaji/ mwombaji.

Katika hatua nyingine Msaidizi wa Asskofu Mch. Deogratius Msanya alimkabidhi Kadi ya pongezi Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Shoo kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti wa Jumui ya Kikristo Tanzania (CCT)

Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumui ya Kikristo Tanzania (CCT) kwenye Mkutano Mkuu wa 31 wa Jumuiya hiyo uliofanyika mkoani Morogoro kwenye Kituo cha Mafunzo ya Wanawake cha CCT tarehe 08-09 Julai 2021.

Katika uchaguzi huo Askofu Shoo alichaguliwa kwa kura 63 kati ya kura 212 zilizopigwa na kuwashinda wagombea wenzake Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Mount Kilimanjaro aliyepata kura 50, aliyekuwa mwenyekiti Askofu Dkt. Alinikisya Cheyo wa Kanisa la Morvian Tanzania aliyepata kura 47.

Wengine ni Askofu Dkt. Mahimbo Mndolwa Mkuu wa Kanisa la Anglikana kura 29, Askofu Mussa Mwageswele wa Kanisa la Afrikan Inland Church Tanzania (AICT)kura 23.

Baada ya uchaguzi wa Mwenyekiti Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro alichaguliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa Kwanza kwa kupata kura 86, akifuatiwa na Askofu Dkt. Cheyo kura 62, Dkt. Mndolwa kura 40 na Askofu Mwageselwa kura22.

Makamu wa pili wa mwenyekiti alichuguliwa Askofu Dkt. Cheyo aliyepata kura 84 akimshinda Askofu Dkt. Mndolwa aliyepata kura 66 na Askofu Mwageselwa kura 57.

Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, akimkabidhi kadi ya pongezi Askofu Dkt. Shoo baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCT.