Warsha Kuhusu Masuala ya Kodi kwa Viongozi wa Dini ( InterFaith)

MKUU wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Interfaith Mkoa wa Kilimanjaro- inayojumuisha viongozi wa dini ya Kikristo (CCT, TEC na TAG) na dini ya Kiislamu BAKWATA; amefungua warsha ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu masuala ya kodi.

Akifungua warsha hiyo ya siku moja iliyofanyika Lutheran Uhuru Hotel & Conference Centre. Ask. Dkt. Shoo alisema, “warsha hii inalenga kutukumbusha na kutujengea uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya Kodi kwa sisi viongozi wa dini, ili tuwe na sauti ya pamoja katika kusimamia ipasavyo rasilimali za nchi, ikiwa ni pamoja na wajibu wa kulipa, kufuatilia matumizi yake na pia kupaza sauti kuhusu mfumo mzima wa ukusanyaji Kodi. Iwe ni katika ngazi ya kitaifa na kimataifa”.

Ask. Shoo aliendelea kusema kwamba, “suala la Kodi ni suala la kisera na kisheria, sambamba na sisi viongozi wa dini kupaza sauti, ni wajibu wa wawakilishi wetu katika Bunge ambalo ndio chombo chetu wananchi katika kutunga na kusimamia sheria na kuiwajibisha serikali kwa niaba yetu. Kwamba wanawajibu muhimu wa kushiriki vyema michakato yote ya mabadiliko ya sera na sheria za kodi za kitaifa na kimataifa. Hii ni pamoja na kuhimiza serikali kupanua wigo wa Kodi kwa manufaa ya wananchi ambao kwa kweli tunapaswa kulipa Kodi kwa furaha, bila vitisho ama bughudha yoyote”

Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi. Ask. Shoo alisema, ” ni matarajio yake kwamba, baada ya warsha hii, washiriki wataweka maazimio ya pamoja katika kuhakikisha rasilimali za nchi ikiwemo kodi zinatungiwa sera na sheria rafiki za utoaji na ukusanyaji na kisha zinatumika ipasavyo kuboresha maisha ya wananchi”.

Ask. Dkt. Shoo alimalizia kwa kutoa Kongole kwa Mratibu wa warsha hii Mch. Andrew Munisi ambaye ni Ofisa Programu wa ELCT ND/NCA.