Wastaafu wakutana Faragha

Wachungaji wastaafu zaidi ya 60 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini wamekutana katika faragha yao iliyofanyika katika hosteli ya  Umoja Lutheran Hostel kuanzia Novemba 8 hadi 11, 2022. Neno Kuu lilikuwa “Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Eee Mungu usiniache”(Zab 71 :18)

Katika Faragha hiyo mbali na mapumziko wastaafu hao walijifunza na kujadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na; Afya yangu iliyowasilishwa na wataalamu wa Afya kutoka Hospitali ya rufaa ya KCMC sanjari na upimaji wa afya kwa baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza. Mada nyingine ilihusu changamoto za hudumu leo na utatuzi wake. 

Akizungumza na  wastaafu hao wakati wa ufunguzi Novemba 9, 2022, Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliwakaribisha wastaafu hao katika maburudisho yao na kuwaambia kuwa hiyo ni nafasi yao kutafakari kwa pamoja juu ya wema wa Mungu ambao ametupa kuwepo hai hadi sasa.

Alisema katika faragha yao wanatarajia kupata  ushauri kutoka kwao na kueleza yale ambayo wanaona yanaenda vizuri na yale wanayotamani kuona yanafanyika.

“Sisi tunatambua kuwa ninyi ni wa thamani kubwa na mmekuwa mnatubariki kwa njia nyingi kwa kutuombea, mnaliombea kanisa la Mungu, mnaiombea sana dayosisi yetu, mara chache chache napokea simu, hata barua fupi tuu ambazo zinasema Askofu tunawaombea, tunawatia moyo songeni mbele na kazi ya Bwana, hiyo inatubariki sana, ninawashukuru”.Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Alsema wanatambua kwamba wamechangia kuweka misingi kwa yale yanayoendelea katika huduma mbalimbali zinazotolewa na Dayosisi na kusema wataendelea kuwathamini.

Aidha aliwashukuru wazee kwa niaba ya Dayosisi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika utumishi wao na kuwaomba watumie nafasi hii kupumzika, kuburudika na zaidi kuliombea Kanisa na wajibu wa viongozi katika Kanisa.

Katika Itikio lililotolewa na Mch. Ngowi kwa niaba ya wachungaji wastaafu alisema wataendelea kuliombea kanisa ili lishike nafasi yake na heshima yake ikapate kuendelea.

 Alimshukuru Baba askofu na uongozi kwa niaba ya wastaafu kwa fursa waliyotoa yakuwawezesha kukutana katika faragha yao na jinsi wanavyowatunza na kuwathamini wastaafu.

“Tunajisikia furaha na amani kwa jinsi mnavyoendelea kutujali, tutaendelea kuwaombea viongozi na Kanisa ili liweze kutekeleza yale Mungu aliyoyakusudia”.Alisema Mch. Ngowi.

Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo akizungumza na wachungaji (wastaafu) kwenye faragha yao Novemba 9, 2022 Umoja Lutheran Hotel