WOINDE NKYA KINARA TUZO YA MWANAMKE WA MABADILIKO

MTAWA wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Woinde Nkya, aibuka kidedea katika tuzo za wanawake wa Tanzania, wenye mchango mkubwa katika jamii.Woinde, anayefanya kazi katika Kitengo cha Building a Caring Community (BCC) kilichoko chini ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini aliibuka kinara wa tuzo hiyo siku chache zilizopita, baada ya kuingia katika kinyan’ganyiro hicho wakiwa wakawake 50. Alitangazwa mshindi wa tuzo iliyoandaliwa na mashirika ya kiraia, baada ya kubaini ndiye mwanamke mwenye mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko katika jamii yao, wakaamua kuwatambua na kuwapa heshima.

BCC, ni Kitengo chini ya Idara ya Udiakonia, kinachotoa huduma na usaidizi kwa watoto wenye ulemavu wa akili pamoja na kusaidia familia zao. Baadhi ya huduma zinazotolewa ni pamoja na matibabu, elimu na mazoezi ya viungo.Mtawa Woinde, ni mtaalamu wa mazoezi tiba (Occupational Therapist), ambaye huweka mpango wa matibabu ya kila mmoja kwa watoto 250, ambao walisajiliwa katika mpango huo.

“Bado matamanio yangu ni kuona kunakuwepo mfumo mzuri na rafiki, ambao utaboresha maendeleo ya mazoezi tiba kwa kila mtoto. Tuzo hii ni heshima kwangu, BCC na Kanisa kwa ujumla,” alisema Mtawa Woinde

Mtawa huyo alitangazwa rasmi kuwa kinara wa tuzo hiyo kwa mwaka 2024, Machi 8 Mwaka huu katika Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alikabidhiwa tuzo hiyo ya wafanya mabadiliko katika jamii, kama sehemu ya shughuli ya siku ya kimataifa ya wanawake.

Alimshukuru Mungu kwa kumuongoza katika safari hiyo, na kushukuru kwa nafasi ya kutambulika kwa jamii yake, lakini muhimu zaidi kwa kila aliyemuunga mkono katika kazi yake.