Yerusalemu: Jimbo la Hai latoa misaada ya Chakula


Kilo 2000 za mahindi na  600 za maharage zimegawanywa kwa kaya zaidi ya 150, zinazokabiliwa na njaa katika Usharika wa Kia mtaa wa Yerusalemu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kijiji cha Tindigani kata ya Kia.

Pia walitoa kilo 500 za mahindi na kilo 100 za maharage katika shule ya msingi Lerai wilayani Hai.

Msaada huo umetolewa na Jimbo la Forchheim  la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Ujerumani ambalo ni jimbo rafiki la jimbo la Hai la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Januari 19, 2022.

Zoezi la ugawaji chakula lilifanywa na Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Mallya na mwakilishi wa masuala ya Elimu Afrika kutoka Jimbo la Forchheim Ujerumani Dkt. Topf Wolfgang.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa chakula Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Mallya amesema kumekuwa na ukame kwa mda mrefu katika eneo hilo ambao umeathiri uchumi .


Anasema watu wengi katika eneo hilo wanategemea mifugo kupata nyama, maziwa na pesa ya chakula . “Binafsi nimeona wanyama wengi wamekufa na hii imesababisha wanaume wengi kuhama kutafuta sehemu yenye malisho, pia imesababisha changamoto ya njaa katika eneo hili na katika maeneo mengine matano ya misioni katika Jimbo la Hai” Alisema Mch. Mallya


Aidha aliwashukuru marafiki kutoka jimbo la Forchheim la Ujerumani  kwa msaada waliotoa  fedha kuwezesha kununua mahindi na maharage.

Mtaa wa Yerusalemu

Mtaa wa Jerusalemu ni moja ya mitaa ya Usharika wa Kia Jimbo la Hai la Kanisa. Kwa sasa mtaa wa Yerusalemu wanaasali chini ya mti wakisubiria jengo la Kanisa likamilike walaau kupauliwa kuondokana na  adha ya upepo, jua na mvua wakati wa Ibada.

Eneo la hili ni mithili ya jangwa lina upepo mkali, jua kali na wakazi wa eneo hili wengi ni jamii ya Wamasai wanaojishughulisha na ufugaji wa ngombe na mbuzi.


Mkuu wa Jimbo anasema ukiacha changamoto ya njaa zipo changamoto nyingine kama kukosekana kwa nyumba ya Ibada katika mtaa wa Yerusalemu na Bondeni. “Katika Usharika wa Kia kuna maeneo mawili yasiyo na nyumba ya Ibada, eneo hili la Yerusalemu na eneo lingine la Mtaa wa Bondeni” Alisema Mch. Mallya.
Hata hivyo Mch. Mally amesema ofisi ya Jimbo imeanza ujenzi wa nyumba ya ibada katika mtaa wa Yerusalemu.