Zaidi ya Wainjilisti 380 wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini wakutana LBS Mwika

Ni tukio la kihistoria, ndivyo tunavyoweza kuandika, kwani ni baada ya takribani miaka ishirini kwa mujibu wa baadhi ya washiriki ambao ni wainjilisti kutoka katika Majimbo yote matano ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini!

Wainjilisti 384, kati yao wanawake 124 sawa na 34% na wanaume 260 sawa na 66% kutoka katika sharika 171 za KKKT Dayosisi ya Kaskazini, walikutana tarehe 6-9 Septemba, 2023 katika Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika kwa semina ya siku tatu.

Semina hiyo iliratibiwa na Idara ya Misioni na Uinjilisti ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini ambayo Mudiri wake ni Mhe. Msaidizi wa Ask. Mch. Deogratius Msanya. Semina hii ni sehemu ya mpango wa Dayosisi wa kuimarisha uinjilisti katika Dayosisi na kuwajengea uwezo wa utoaji taarifa, kuwapatia maarifa na ujuzi watumishi wa kada ya Uinjilisti katika Dayosisi. Aidha, ni fursa pia ya watumishi hawa kushiriki pamoja Neno la Mungu, kuomba, kuimba n.k

Ifahamikwe kwamba, katika kipaumbele cha uendelevu wa Kanisa katika Mpango Mkakati wa Dayosisi 2023-2027, Dayosisi imejiwekea malengo ya kukua kwa idadi ya washarika wapya zaidi ya 160,000 kwa kipindi cha miaka mitano. Kukua huku, kutatokea kupitia uinjilisti kwa kuwa na mikutano ya wazi, nyumba kwa nyumba, makundi maalumu, kadhalika kupitia majukwaa ya kidijitali hususan mitandao ya kijamii.

Akifungua semina hiyo, Mhe. Askofu Dkt. Shoo aliwapongeza wainjilisti kwa kupata fursa ya kukutana pamoja kwa lengo la kujengeana uwezo na kuimarishana katika huduma. Aliwaambia kuwa huduma yao imekuwa ya baraka na ni uti wa mgongo kwa Dayosisi na Kanisa kwa ujumla. Alisema kuwa, huduma yao katika ustawi wa Kanisa ni ya muhimu sana na kuwataka kuitumia fursa hiyo ya kukutana kujadilia mambo mbalimbali katika utumishi yatakayosaidia kujenga na kuendeleza Kanisa.

Akirejea somo la ufunguzi kutoka kitabu cha 2 Wakorintho 4:1-9 lisemalo, “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei; lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika……”

Ask. Dkt. Shoo alisema kwamba, ni muhimu na lazima kwa watumishi wa Kanisa kuzingatia sana neno lisemavyo; kuwa imara katika huduma na kufundisha kweli ya Neno la Mungu bila kulegea na kutambua kuwa huduma hii wamepewa kwa neema tu.

Aliendelea kusema,“Ninyi ni wahudumu wa zama hizi mpya na mmepewa kazi hii kwa rehema na kwa Neema ya Mungu; Neno la Mungu linawakumbusha msije mkajisahau kwamba mnastahili kuwa katika hii huduma, ni kwa neema tu. Mtumishi wa Mungu anapojisahau na kufikiri kwamba anastahili; Shetani anajiinua na kumpa kiburi na mwisho analegea katika huduma”.

Pia aliwataka watumishi hao kujihadhari sana na tabia ya kulichanganya Neno la Mungu na uongo. Alisema wanapaswa kulihubiri Neno la Mungu katika usafi na usahihi wake ili watu wa

Mungu waimarishwe kiimani kwa taarifa na maarifa sahihi kuhusu Neno la Mungu na maisha ya ufuasi hususan kwa kuzingatia tafsiri na mikazo ya Kilutheri. “Mafundisho ya utajirisho yanapotosha ukweli wa Neno la Mungu. Badala ya kufundisha watukufanya kazi kwa bidii, baadhi ya watumishi wanawafundisha kupokea tu katika ndoto bila kuwaelekeza watu kufanya kazi kwa bidii huku wakimwomba na kumtegemea Mungu.”

Mhe. Ask. Dkt. Shoo alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza wainjilisti ,kutafakari mafundisho yanayofundishwa na kutambua yanalenga wapi . “Wakristo wengi wamerudi kule walipokuwepo wazee wetu kabla ya Ukristo, wanapewa maji, vitambaa, mafuta n.k., huu ni kama ushirikina. Fundisheni, onyeni watu ili waweze kulifahamu Neno la Mungu na ukweli wake wote ili waweze kuepuka mafundisho potofu”. Alisema Dkt. Shoo.

Naye Mwinjilisti Kaveja kwa niaba ya Wainjilisti wote, alimshukuru sana Ask. Shoo kwa mafundisho na nasaha alizowapa na alishukuru Dayosisi kuandaa semina hiyo muhimu na alimpongeza kwa jitihada zake za dhati za kusimamia Injili katika Kanisa. Alisema, “Sisi Wainjilisti tunakushukuru sana kwa kutupa fursa hii ya kukutana pamoja, jambo ambalo halikufanyika kwa takribani miaka 20.” kauli ambayo ilisindikizwa kwa makofi mengi kutoka kwa washiriki.

Aidha, Mwinjilisti Kaveja, alihitimisha kwa kusema, “Tumefurahi na tumeguswa na maono ya Dayosisi ya kuwezesha semina hii. Sisi kama Wainjilisti tutatekeleza kwa uaminifu yale yote uliyoelekeza na kuasa. Tutayafanyia kazi na kuwa na subira kwa yale mazuri yaliyopangwa kwa ajili yetu”, alihitimisha.