Mwanga Mpya Kaskazini: Hope International na KKKT Wasaini Mkataba wa Kuinua Maisha ya Waumini

“Hope International na KKKT Dayosisi ya Kaskazini Wasaini Makubaliano ya Ushirikiano (MOU)” ;

Msaidizi wa Askofu  atoa pongezi

Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Deogratius Msanya, ameishukuru Hope International kwa juhudi zake za kusaidia jamii kuinuka kiuchumi na kiroho.

Akizungumza katika uzinduzi na utiaji Saini ya Makubaliano-Memorundum of Understanding (MoU) ya mradi  huo wa Ushirika wenza baina ya Hope International na KKKT Dayosisi ya Kaskazini, amesema mpango huo ni wa maono mazuri na utaleta nuru mpya kwa Dayosisi ya Kaskazini pamoja na kuwapatia waumini tumaini jipya la maisha bora.

Utiaji Saini huo umefanyika leo Aprili 10, 2026 kwenye Ukumbi wa Uhuru Lutheran Hotel

Amesisitiza umuhimu wa vikundi vya akiba, akibainisha kuwa fedha nyingi hupotea mikononi mwa watu kutokana na kukosa maarifa ya usimamizi wa fedha.

Akinukuu mafundisho ya Biblia, amesema watu wanaangamia kwa kukosa maarifa, hivyo elimu ya kifedha inayotolewa na Hope International ni muhimu katika kuleta mabadiliko chanya.

Aidha, amesema mpango huo unalenga kumkomboa mtu kiroho na kiuchumi, na amewahimiza wasimamizi wa mradi huo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na umakini ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika tathmini zijazo.

Ameongeza kuwa mpango huo ni wa kipekee kwani unajenga imani ya mtu na kumuwezesha kujitegemea kiuchumi.

Amesisitiza kuwa mafanikio yanahitaji kumtumikia Mungu na kufanya kazi kwa bidii.

Pia amegusia matumizi makubwa yasiyo ya lazima, hususan kwenye sherehe, akieleza kuwa elimu inayotolewa itasaidia kubadili mtazamo wa matumizi ya fedha na kuhimiza uwekezaji wenye tija.

Mpango huo umeanza katika majimbo

mawili, huku matarajio yakiwa ni kupanuka zaidi na kuwafikia watu wengi zaidi nchini.