KATIBU MKUU KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI AWEKA JIWE LA MSINGI KUSHEREHEKEA MIAKA 20 YA KUSIRYE-U

KATIBU Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mhandisi Zebadiah Moshi, ameweka jiwe la msingi la kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Shule ya Msingi ya mtaala wa Kiingereza ya Kusirye-U.

Tukio hilo limefanyika Jumamosi, Septemba 5, 2026, katika eneo la shule hiyo, na limeambatana na sherehe za mahafali ya wanafunzi wa Darasa la Saba.

Uwekaji wa jiwe la msingi umetanguliwa na ibada ya shukrani, ambapo Mchungaji Fadhili Kiwera amewahudumia waliohudhuria kwa Neno la Mungu pamoja na maombi ya kumshukuru Mungu kwa hatua hiyo ya miaka 20 ya shule.

Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa Shule ya Kusirye-U, waasisi wa shule hiyo, viongozi wa serikali, wachungaji, viongozi kutoka KKKT Dayosisi ya Kaskazini pamoja na wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo wazazi.

Baada ya kuweka jiwe la msingi, Katibu Mkuu, Mhandisi Zebadiah Moshi, amekagua gwaride la Skauti kama heshima kwake akiwa mgeni rasmi wa sherehe hizo za mahafali ya Darasa la Saba zilizofanyika siku hiyo.

Sambamba na sherehe hizo, wanafunzi waliohitimu Darasa la Saba wamekabidhiwa vyeti vyao na Katibu Mkuu, Mhandisi Moshi.

Katika kuonesha heshima na kutambua mchango wake katika siku hiyo pamoja na maendeleo ya shule kwa ujumla, uongozi wa Shule ya Kusirye-U umemkabidhi Mgeni Rasmi zawadi ya saa.

Aidha, baadhi ya waasisi wa shule hiyo wamekabidhiwa vyeti vya kutambuliwa na Mgeni Rasmi kabla ya kuhitimishwa kwa sherehe hizo.