MOSHI, KILIMANJARO: Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini na Dayosisi ya Kaskazini Kati, wamekutana katika makao makuu ya Dayosisi ya Kaskazini, mjini Moshi, kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala ya rasilimali watu, uchumi na uongozi wa Kanisa.
Mkutano huo umefanyika leo, Oktoba 1, 2026, katika ukumbi uliopo kwenye ofisi za Dayosisi ya Kaskazini, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kushirikisha viongozi kutoka dayosisi hizo mbili.
Akizungumza katika mkutano huo, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Deogratius Msanya, amewakaribisha viongozi kutoka Dayosisi ya Kaskazini Kati -Arusha na kuwafikishia salamu za Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Shoo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Mhandisi Zebadiah Moshi, ameukaribisha uongozi huo kutoka Arusha na kutoa maelezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mfumo wa uongozi na utendaji wa Dayosisi ya Kaskazini.
Akizungumzia manufaa ya mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Mipango, Fedha na Utawala wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, CPA Mussa Masanga, amesema kuwa wamejifunza mambo mengi kupitia zoezi hilo la kubadilishana uzoefu. Pia ametoa shukrani kwa uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini kwa mapokezi mazuri na maandalizi ya mkutano huo.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru ofisi ya Mheshimiwa Katibu Mkuu kwa mapokezi mazuri na namna ambavyo wameratibisha zoezi zima hili la kubadilishana uzoefu. Tumejifunza mengi sana na tunabeba salamu nyingi sana za upendo na ukarimu wenu kurudisha kwenye Dayosisi ya Kaskazini Kati,” amesema CPA Masanga.
Naye Afisa Rasilimali Watu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Edith Mkisi, ameishukuru Dayosisi ya Kaskazini kwa kutoa fursa hiyo ya kubadilishana uzoefu. Amesema anaamini kuwa mambo aliyojifunza kupitia mkutano huo yatasaidia kuboresha utendaji wa kazi katika Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Dayosisi ya Kaskazini, Mercy Matemu, amemshukuru Mungu kwa kufanikisha mkutano huo na kueleza kuwa wanatarajia kuona matokeo mazuri katika hatua zitakazofuata.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za viongozi wa dayosisi hizo mbili katika kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kiutawala, rasilimali watu na uchumi wa kanisa.

