HABARI YA KONGAMANO LA VIJANA JIMBO LA MASHARIKI

Mamia ya vijana waliohudhuria Kongamano la Vijana la KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, wamefanya uamuzi wa kumpokea Yesu Kristo na kuanza maisha mapya ya imani.

Kongamano hilo limefanyika Novemba 16, 2026, katika Usharika wa Himo Mjini, likiwakutanisha maelfu ya vijana kutoka ndani na nje ya jimbo hilo kwa ajili ya kusifu, kuabudu na kupokea mafundisho ya kiroho.

Akitoa neno la kongamano hilo, Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, Mchungaji Calvin Koola, ametumia kauli mbiu isemayo “Mtu asiudharau ujana wako”, akiwahimiza vijana kutumia vizuri kipindi cha ujana kwa kujenga tabia njema na kuwa na mwelekeo chanya katika maisha yao.

Mchungaji Koola amesisitiza umuhimu wa vijana kutambua thamani ya muda walionao na kuutumia kwa mambo yenye tija. Aidha, amewaonya dhidi ya kujihusisha na udanganyifu katika mahusiano ya kimapenzi yasiyo na mwelekeo wa ndoa na yanayokiuka misingi na taratibu zinazofaa.

Mbali na mafundisho ya kiroho, kongamano hilo limewapa vijana nafasi ya kushiriki katika nyimbo za sifa na kuabudu, kucheza pamoja na kufanya maombi ya pamoja, hali iliyochangia kuimarisha ushirika na mshikamano miongoni mwao.

Katika hatua nyingine, Mchungaji Koola amezindua rasmi Tamasha la Funga Mwaka Na Yesu 2026, lenye kauli mbiu isemayo “Maono Yangu, Hatima Yangu”. Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Desemba 19, 2026, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.