ASKOFU SHOO AWEKA MAWE YA PEMBE KATIKA MAJENGO MATATU YA IBADA NA HUDUMA JIMBO LA HAI

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameweka mawe ya pembe katika majengo matatu tofauti ndani ya Jimbo la Hai, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza huduma za kiroho na kuboresha mazingira ya ibada kwa waumini.

Matukio hayo yamefanyika Novemba 22, 2026, ambapo Askofu Shoo alianza kwa kuweka jiwe la pembe katika jengo la Nyumba ya Utulivu (Retreat Centre), lililopo katika Usharika wa Hai Mjini.

Baadaye aliweka jiwe la pembe katika jengo la ibada lililopo Mtaa wa Miembeni, kabla ya kuhitimisha ziara hiyo kwa kuweka jiwe la pembe katika jengo la ibada la Mtaa wa Ewang’any, chini ya Usharika wa Hai Mjini.

Katika Mtaa wa Miembeni, ilielezwa kuwa jengo hilo awali lilikusudiwa kutumiwa na watoto wa shule ya Jumapili (Sunday School), lakini baada ya kukamilika litatoa huduma pia kwa wazazi na wazee ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya umbali kufika katika Usharika wa Moshi Mjini kwa ajili ya ibada.

Akizungumza katika matukio hayo, Askofu Shoo amepongeza mawazo na jitihada za waumini katika kuanzisha na kusimamia miradi hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza moyo wa uaminifu katika usimamizi wa ujenzi ili majengo hayo yakamilike kwa ubora na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Katika Mtaa wa Ewang’any, uwekaji wa jiwe la pembe umepokelewa kwa furaha na waumini ambao wameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kupunguza changamoto ya umbali wa kufika katika nyumba za ibada na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiroho karibu na makazi yao.

Aidha, akiwa katika ibada ya uwekaji wa jiwe la pembe katika Mtaa wa Ewang’any, Askofu Shoo ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo hilo, ambapo fedha taslimu pamoja na ahadi zilizotolewa zimefikia thamani ya zaidi ya shilingi milioni 45.

Katika ziara hiyo, Askofu Shoo ameambatana na viongozi mbalimbali wa Dayosisi ya Kaskazini pamoja na Askofu kutoka Dayosisi ya Stockholm, Kanisa la Sweden, walioshiriki katika matukio hayo ya uwekaji wa mawe ya pembe.