ASKOFU DKT. FREDRICK SHOO AZINDUA MTAA WA EBENEZER

Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Shoo, amezindua mtaa wa Ebenezer katika Usharika wa Bashay Jimbo la Karatu, ni mara baada ya washarika hao kukaa katika jengo dogo la Kanisa zaidi ya miaka kumi.

Mapema wiki hii Askofu Dkt. Shoo wakati akizundua mtaa huo, ameshangazwa na jinsi ambavyo Wakristo wa Usharika wa Bashay walivyo na  moyo wa utoaji katika kumtumikia Mungu na kushiriki vyema katika shughuli za umoja katika Kanisa.

Aliendelea kusema, licha ya kwamba washarika hao wamefanya kazi kubwa, hatuna budi kuwashukuru marafiki zetu kutoka Finland ambao wamejumuika pamoja kuchangia zaidi ya Milion Sitini kati ya Milioni Tisini zilizotumika kukamilisha ujenzi.

“Jimbo la Karatu lilianza kama Misioni tu, ilikuwa kama Usharika mmoja au sharika mbili na kwenye risala tumesikia mtaa huu ulianza na washarika Kumi na Tano na leo kuna zaidi ya washariki Mia na Themanini. Hii ni ishara tosha kwamba, watu wa Mungu wanampokea Kristo na hii ni alama tosha kwamba Kanisa la Mungu linaongezeka”.Alisema Askofu Dkt. Shoo

Alitoa wito kwa Wachungaji, Wainjilisti, Wasaidizi wa Sharika na Kanisa kwa ujumla kushikamana katika kuifanya kazi ya Mungu maadam ni mchana maana usiku waja wa mtu asi weze kufanya kazi.

Naye  Mchungaji Kiongozi kutoka Nchini Finland Usharika wa Mikkeli, Mchungaji Riston alisema, uhusiano wao na sharika za Bashay na Qurus ni upendo wa Mungu kwao, maana haikuwa rahisi kwa Ulaya na Afrika kuwa na urafiki wa jinsi hii.

“ Mwanzoni ilikuwa kama ndoto wakati tunazungumza na Mchungaji Dalei ambaye yeye anatunza uhusiano huu, lakini Waswahili husema kidogo kidogo hujaza kibaba na ndivyo ambavyo imekuwa”. Alisema Riston